6/29/2004

wazungu washenzi kweli

Yaani wazungu wakisikia Afrika wanafikiri ni kama Ethiopia miaka ya 80 au Rwanda wakati wa mauaji ya halaiki. Wanadhani kila kukicha tunakatana mapanga au tunagalagala chini tukisubiri kufa kwa njaa kali. Tazama nchi kama Marekani, watu zaidi ya milioni mbili wako jela, watu zaidi ya milioni 40 hawana bima ya afya (hawa ni wale vibogoyo, kwa mfano, maana hawana hela ya kwenda kwa daktari wa meno!), idadi ya watu wasio na makazi ni kubwa kuliko nchi yoyote ya ulimwengu wa kwanza, watoto wanaoishi ghetto wanakula jumatatu hadi ijumaa chakula kingi maana jumamosi na jumapili nyumbani hakuna chakula, kwa mwaka watu zaidi ya 15,000 wanauawa kwa bunduki, watoto zaidi ya 100,000 wanatekwa...huu ni ulimwengu wa kwanza au wa kumi? Ubepari unaficha mengi. Majumba, sinema, magari, barabara nzuri vinaficha umasikini na unyama wa mfumo huu. Ni kama Afrika Kusini. Majengo mazuri, barabara za kisasa lakini Johannersburg, kwa mfano, inajulikana kama "rape capital of the world." Kila dakika anabakwa mtu! Ukiacha Moscow hakuna jiji lenye uhalifu kama Johannersburg. Lakini tazama mandhari yake.

IRAKI, eti ni nchi huru sasa!

Eti Iraki iko "huru" sasa. Katamka Rais, mwizi wa kura, wa hapa Marekani, Bwana Kichaka (Bush). Hii ni sawa na Afrika Kusini ambako watu weusi wanatawala kisiasa ila nguvu za kiuchumi, ambazo ndizo nguvu halisi, ziko mikononi mwa Makaburu ambao wanainunua Tanzania kwa kasi ya mwanga. Uchumi wa Iraki, ninamaanisha mafuta, uko mikononi mwa makampuni ya Amerika. Ni Wamarekani ambao watakuwa wanatoa maamuzi makuu juu ya sera na biashara ya mafuta. Hii dunia ya uongo, tufanyeje? Nyanyuka mlalanjaa!

6/27/2004


Baba Ukweli na Mama Ukweli na rafiki toka kisiwa cha Martinique (alikotokea Frantz Fanon, yule mwandishi wa kitabu cha Waliolaaniwa). Posted by Hello


Ndesanjo akiwa utelezini barafuni. Toka kuteleza kwa kisigino pale Mpirani, mkoani Kilimanjaro hadi kwenye barafu. Hapa ni nje ya jiji la Seattle, jimbo la Washington Posted by Hello


Wapambanaji wa kundi la kimapinduzi lililotikisa Marekani la Black Panther wakiwa Arusha, Tanzania Posted by Hello


Kila mwaka mji wa Toledo hapa Ohio huwa unasherehekea siku ya Tanzania. Siku hii huandaliwa na shirika la Great Lakes Consortium ambalo hushughulika na miradi mbalimbali ya maendeleo hapo Tanzania. Pia mji wa Toledo ni mji-dada wa mji wa Tanga. Picha hii inaonyesha siku ya Tanzania mwaka juzi, ambapo vinyago na vitu mbalimbali toka Tanzania viliuzwa. Posted by Hello

Utamaduni Msalabani

Hii ni sehemu ya shairi jingine ambalo ni refu kidogo. Nitakupa beti mbili tu. Linaitwa Utamaduni Msalabani.

Kura twapiga, sadaka twatoa
Kodi twalipa, swala twasali
Walalanjaa
Cha moto, mbona
Bado Twakiona?

Demokrasia ghasia
Mafukara twauziwa,
Jehanamu ya moto
Masikini twatishiwa,
Wa kusema wamesema
Wa kusikia ni viziwi,
Hivi chukua chako mapema
Ni azimio la wapi?

AMERIKA

Hili ni sehemu ya moja ya mashairi ambayo yatachapwa karibuni. Linaitwa Amerika:

Hii hapa Amerika
Uliyoililia
Harakaharaka ndio mwendo
Polepole haina baraka
Baridi kali, sheria kali
Utamaduni baridi.

Binadamu wanaongea na mbwa
Wao kwa wananuniana!

6/26/2004

Mlio wa mtutu na sauti ya muazini

Wakati nikiishi Dar, kila asubuhi na jioni nilisikia sauti ya muezzin (muazini) akiita Waislamu wakasali. Niliishi hatua chache toka msikitini (pale Tabata na Mbagala). Sauti ya "Swalaaaa....," ilikuwa ikisikika kama vile anayeomba yuko dirishani. Sasa hapa Marekani, kila jioni na asubuhi nasikia sauti ya risasi na ving'ora vya magari ya polisi na magari ya wagonjwa. Hizi risasi sijaweza kujua zinatokea wapi. Ninahisi kuna kambi karibu na hapa ninapoishi, barabara ya Uwanja wa Ndege, nje kidogo ya mji wa Toledo, Ohio. Ule mti niliosema unanitisha, kuwa unaweza kutuangukia chumbani siku moja, bado upo umesimama. Asubuhi ya leo niliutazama weee....

Unajua Wi-FI kwa kiswahili?

Wi-fi ni mtando wa mhahalishi (internet) ambao hautumii waya wala mnara. Kama una tarakilishi (kompyuta) ya mkononi unaweza kuingia kwenye webu ukiwa popote pale. Kwa kimombo wanaita wireless, lakini kwa kiswahili inaitwa mtandao usiwaya.

6/25/2004

UNAJUA MANENO HAYA YA KISWAHILI?

Kwa sasa watu wanaweza kuwasiliana kwa kutumia

tarakilishi (computer) iliyoungwa kwenye mtandao (network)

kuweza kuvinjari kwenye mdahalisi (internet) ikiwa tu

wanajua anuani ya baruapepe (e-mail) ya wanaemhitaji.


Baruapepe yaweza kuwa kwenye tovuti (website) ambayo

wewe utahitaji kubofya (to surf) tu ili kuipata.

Teknolojia hii imesitisha matumizi ya kinakilishi (fax)

na pia imeongeza kasi ya upatikanaji wa maarifa ya

ujasiliamali (entrepreneurship knowledge) miongoni mwa wafanyabiashara.

Hivi sasa mchakato (process) wa maendeleo duniani unaanza

kuchukua sura tata(complex)kwani kila mahali panatafuta

asasi(resource! ) yake.

Blogu

Nimemaliza kufunza wanafunzi kutengeneza blogu zao. Blogu ina umaarufu sana miongoni mwa matineja. Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC asilimia kubwa ya blogu ni za matineja. Soma habari hiyo hapa.

6/24/2004

Bush na wezi wenzie

Bush na wezi wenzie nasikia matumbo yao moto kutokana na filamu ya Michael Moore iitwayo Fahrenheit 911 ambayo pamoja na mambo mengine inaonyesha uhusiano wa familia ya Bush na Osama na pia wauaji wa Kinazi. Bado sijaitazama ila napanga kwenda wikiendi moja na familia. Kuna siku nilisema kuwa Moore ana kitabu kinaitwa Stupid Whitemen! Kumbuka kuwa yeye naye ni mweupe!

mpira wa miguu au mikono

Kuishi ughaibuni kwenye nchi ambayo watu hawapendi mpira wa miguu (soka) ni jambo baya sana. Ukiongelea mpira wa miguu, football kwa kiingereza, wamarekani wanafikiri unazungumzia american football. Huu ni mchezo wa mabavu, unacheza huku ukiwa umevaa machuma usoni! Jambo ambalo sijaweza kupata ufumbuzi wake ni hili. Kwanini wanauita huu mchezo mpira wa miguu wa kimarekani (american football) wakati asilimia 99.99 ya huu mchezo unatumia mikono? Wauite handball!

6/23/2004

Nimebanwa

Da! Hizi siku mbili tatu huyu mtu mweupe anayekalia hii nchi ya wahindi wa asili (native americans) amenikamata kweli. Unajua tena hii ni nchi ya kodi na bili! Hivyo lazima jasho likutoke. Naona watu wasio na hatia wanaendelea kukatwa vichwa katika aina mpya ya ugaidi.

6/21/2004

Mbingu na jehanamu

Swali: Hivi kwanini unadhani kuwa mbingu au jehanamu utaipata baada ya kufa wkati vyote viko hapa duniani? Usikubali shehe au kasisi akudanganye maisha yako yote. Hoji! Kataa kudanganywa!
Tatizo kubwa ulilonalo ni kudhani kuwa ni kweli kasisi na shehe huwa "wanaongea na mungu."

Hakuna uhusiano kati ya Iraki na Osama!

Tume ya kitaifa inayochunguza tukio la kigaida la Septemba 11, 2001, imesema kuwa hakuna ushahidi kuwa Saddam Hussein alihusika na shambulio hilo. Wamesema kuwa Osama alikuwa na uhusiano wa karibu na nchi za Pakistani (ambayo ni rafiki mkuu wa Marekani), Iran, na Saudi Arabia. Kumbuka kuwa Wamarekani waliambiwa, na wengi waliamini, kuwa Iraki lazima ivamiwe maana ilihusika na shambulio la jengo la World Trade Center. Ushahidi hakuna! Bush na makamu wake Cheney hawajui wajifiche wapi. Kila hoja waliyoitoa inapanguliwa. Habari zaidi soma ukurasa huu.

6/20/2004

Ubepari ndio tunaoutaka?

Mfumo wa uchumi wa kibepari ni kama barabara ya lami mchana wa jua kali. Ukiwa barabarani unaona mbele yako kama vile kuna maji. Kiingereza wanasema hiyo ni mirage. Ndivyo ilivyo hili taifa. Umasikini, hujuma, rushwa, magonjwa ya akili, ukimwi na vitu kama hivyo vimefichika sana. Je unajua kuwa watu milioni 43 hawana bima ya afya? Kama huna bima ya afya katika nchi kama hii wewe ni kama binadamu asiye na uhai!

Ninatazama sinema iitwayo Waco. Unakumbuka lile kundi la dini na Branch Davidians ambalo mwanzo wa miaka ya 1990 lilikuwa na ugomvi na serikali kisha yakatokea mapigano na FBI. Jumba lao liliungua moto. Serikali ilidai kuwa waumini hao waliamua kujiua. Wengine wanadai kuwa serikali iliwaua. Sinema hii inachambua kwa kina tukio hili. Habari zaidi za Branch Davidians nenda hapa

6/19/2004

Adamu na Hawa

Kama Adamu na Hawa walikuwa na watoto wa kiume wawili (Kaini na Abeli), je watoto wa Kaini na Abeli walitoka wapi? Jibu ninalo, ila nakupa changamoto kidogo. Na je tunda la katikati ni lipi? Wengine wanadai kuwa ni tendo la ndoa. Mimi napinga. Hawa alikula kwanza mwenyewe hilo tunda kisha ndio akamshawishi Adamu ajaribu. Adamu naye akala mwenyewe. Je ni tendo la ndoa? Kama sio, ni tunda gani? Changamoto nyingine ya jumamosi ya leo ambayo ni siku ya sabato ya wayahudi.

Clinto alilala sebuleni!

Aliyekuwa Rais wa Marekani, Bill Clinto, alilala sebuleni kwenye makochi kwa zaidi ya miezi miwili baada ya kukubali mbele ya mke na mtoto wake kuwa alikuwa na uhusiano wa siri wa kimapenzi na Monica Lewinsky. Kama ingekuwa ni kiongozi wa Tanzania, nadhani mke ndiye angelala sebuleni. Au angerudishwa kwao, pamoja na kuwa mwenye makosa ni mume! Clinto ametoa siri hii ndani ya kitabu chake kipya kiitwacho My Life. Habari zaidi soma hapa.

6/17/2004

Blogu ya K.Y. Amoako wa ECA

Katibu Mkuu wa Economic Commission for Africa, K.Y.Amoako naye ana-blogu. Itembelee blogu yake hapa.

Jimmy Carter Blogging from Afrika

Ulijua kuwa Jimmy Carter, Rais wa zamani wa Marekani, alikuwa ana-blogu toka Afrika alipoitembelea? Bonyeza hapa usome.

usisahau

Nimemaliza kutuma makala ya mwisho katika mfululizo wa makala juu ya imani ya Kirasta. Kwahiyo usisahu kusoma jumapili hii katika gazeti la Mwananchi (gumzo la wiki).

6/16/2004

Vitabu vya Nyerere

Siku hizi naulizwa maswali makali makali juu ya Tanzania. Nimeulizwa, "Hivi vitabu alivyoandika Mwalimu Nyerere vinatumiwa shuleni?" Jibu ni kuwa sijui. Sidhani. Kwa jinsi ninavyojua nchi yangu, sidhani. Utasikia watu wakisema Nyerere Baba wa Taifa lakini ukiwauliza maana yake ni nini hasa midomo inacheza. Watanzania kama taifa bado tunacheza. Sijui ni jambo gani ambalo tunalifanya kwa uhakika na makini. Watu wa maneno meeeeeengi. Tunapenda maneno sana. Tunakwenda kwenye mikutano ya siasa. Wanasiasa wanatuuzia maneno. Tunashangilia kweli na kuwachezea ngoma na kuimba huku tukiungua jua. Wao wako kivulini. Waongo wote. Sio wa upinzani. Sio watawala. Waongo watupu.

Kichaka

Vyombo vya habari hapa vinazungumzia sana juu ya madai kuwa Rais Mugabe wa Zimbabwe aliiba kura. Nashangaa kwanini hawasemi pia kuwa huyu rais Kichaka (jina lake kwa kiswahili) aliiba kura! Sasa wizi wa kura utaanzwa kufanywa kwa kutumia teknolojia. Kampuni ya Diebold imetengeneza mfumo wa kupiga kura kwa njia ya electroniki (kwa kutumia mdahalishi). Kampuni hii huwa inatoa fedha nyingi kukiunga mkono chama cha Rais Kichaka cha kihafidhina. Na kampuni hii itakuwa inajua siri ya kuweza kubadili mahesabu na hakuna mtu atakayeweza kuthibitisha. Pia kama kuna utata juu ya idadi ya kura kama ilivyokuwa kule California, hakuna namna ambayo watu wanaweza kuthibitisha kuwa walipiga kura.

Kuna wizi mwingine wa kura wa kijanja sana. Ukiwa jela au ukiwa uliwahi kufungwa huna haki ya kupiga kura. Kwakuwa wafungwa wengi ni wanaume weusi. Na watu wengi walioko jela ni masikini maana matajiri huwa hawaendi jela. Kwanza wana uwezo wa kupata mawakili wa hali ya juu kabisa. Pili, wanakutana na viongozi wa nchi, majaji, na wanasiasa katika viwanja vya gofu, majumba ya kufanyia mazoezi, kwenye sherehe, baharini wakivua samaki, klabu za kucheza mchezo wa darts . Wanaishi katika dunia moja na watunga sheria, watafsiri sheria, na wakamataji wahalifu.

Kwakuwa basi watu wengi wenye rekodi za kufungwa ni weusi na wazungu wachache masikini. Na kwakuwa masikini wengi hawakipendi chama cha Conservative kutokana na rekodi yake ya upendeleo zaidi kwa matajiri. Chama hiki kinaunga mkono sheria hii ya kuwa wafungwa wasipige kura maana wanajua kuwa masikini hawa walioko jela au waliokuwa jela wakiruhusiwa itakuwa ni sawa na kuwapa chama cha Democrat kura zaidi. Ukienda California, katika kila watu weusi watano, watatu hawaruhusiwi kupiga kura. Yaani kuna binadamu hawana haki ya kupiga kura kabisa hapa duniani. Kura ni kati ya haki ambazo ukinyima mtu unakuwa umefika hatua ya juu sana katika udikteta. Udikteta huu ni mbaya kweli, ila hauonekani kwa urahisi. Ndio maana watu wengi tukiongelea viongozi wala rushwa tunataja viongozi wa nchi masikini, kumbe nchi tajiri rushwa imefichwa sana. Huioni kwa urahisi. Kwanini? Sababu kubwa ni kuwa rushwa katika nchi kama ni kubwa sana. Kwahiyo ukiona mtu anasema hapa hakuna rushwa ujue huyo mtu ni masikini. Masikini hawahusiki na rushwa kwa wingi kama matajiri. Lakini hata hapo Tanzania tunajua kuwa sisi masikini tunaweza kudhani kuwa viongozi wetu hawachukui rushwa. Utajuaje wakati hawawezi kuja kuchukua rushwa kwako? Wanachukua kwa wale wenyenazo.

Ninachosema ni kuwa wizi wa kura hapa katika nchi ya KIchaka umehamia kwenye kompyuta na sio masanduku ya kura tena.

umoja wa Afrika?

Hivi huu "umoja wa Afrika" ni umoja wa viongozi wa Afrika au ni umoja wa wananchi wa Afrika? Hakuna mwananchi hata mmoja ninayekutana naye toka Afrika ambaye anazungumzia umoja huu. Hakuna anayeonekana kujali. Kila mmoja anaona kuwa umoja wa Afrika ni kama chama cha viongozi, mawaziri, na wasomi. Ni nafasi nyingine ya watu hawa kuwa na vikao visivyoisha na matamko yasiyo na vitendo.

risasi

Nasikia milio ya risasi. Utafikiri mitutu iko kando ya dirisha. Sijui kuna kambi ya jeshi hapa karibu. Kila usiku ni risasi tu. Ni wanajeshi wako mazoezini au ni magenge?

Sijawahi kusikia milio ya risasi na kuona bunduki nyingi namna hii maishani mwangu. Kila askari unayekutana naye hapa lazima ana bunduki. Kwanza sio askari tu, katiba ya nchi hii inatoa haki ya kila raia kubeba silaha. Hivi karibuni jiji la Toledo limepitisha sheria ya kuruhusu wakazi wake kubeba silaha hadharani. Sitagombana na mtu hata siku moja. Unagombana na mtu kumbe hazimo, mara bastola, mara risasi...na imetokea mara nyingi sana.

6/15/2004

Ujambazi na maendeleo

Utashangaa kuwa Tanzania "inavyozidi kuendelea" ndivyo ambavyo ujambazi wa kutumia silaha utakavyokuwa ukiongezeka. Lazima basi kuna tatizo katika tafsiri yetu ya maendeleo. Tazama Afrika Kusini. Hii ndio nchi pengine ya kwanza kwa uchumi wenye nguvu na "maendeleo" barani Afrika lakini ndio nchi inayoongoza kwa uhalifu, mauaji, ubakaji, na wingi wa nyumba za maboksi!

Wezi tunawaua au kuwakata mikono kama gazeti linavyosema SOMA HAPA! Wezi wa shilingi 1000 pale Manzese tunawau. Wanaotuibia mamilioni na mali asili ya nchi tunawafanya nini?

Utajiri wa Marekani

Asilimia 10 ya Wamarekani wanamiliki asilimia 85 ya utajiri wote wa nchi unaouona kwenye luninga. Kuna asilimia 0.1 tu ya Wamarekani ambao wana kipato cha dola milioni moja kwa mwaka.

Moja ya siri ya ubepari duniani ni kufanya watu wadhani kuwa majengo mazuri, magari, mahoteli makubwa, barabara nzuri ni vigezo vikuu vya maendeleo.

Rafiki yangu mkubwa hapa Marekani amepatikana na ugonjwa uitwao MS. Karibu achanganyikiwe maana hakuna kampuni ya bima inayokubali kumpa bima maana hana kipato cha kutosha. Amegutuka kuwa kumbe kuishi katika nchi tajiri hakuna maana kuwa wewe nawe ni tajiri.

Alitembelea Cuba hivi karibuni. Anasema ameshangaa kuwa CUba inadaiwa kuwa ni nchi masikini wakati ambapo nagekuwa CUba angetibiwa bure maisha yake yote.

Sijui nilikuwa nataka kusema nini hasa katika blogu hii. NImeamka kwahiyo kichwa hakijakaa vizuri. NI saa nane na dakika kadhaa usiku. Ngoja ninawe uso.

ujumbe wa leo

ASIYEJUA HISTORIA NA UTAMADUNI WAKE NI SAWA NA MTI USIO NA MIZIZI.
- Maneno ya Marcus Mosiah Garvey (yohana mbatizaji wa watu weusi).

Jamani msinirarue

Naona kuna watu wamenijia juu kweli baada ya kusema kuwa nimewaambia wanafunzi kuwa bado Afrika tunaishi juu ya miti. Shekya naona habari imekukuna sana. HAMTAKI UTANI? Nilikuwa natania. Nilisema kuwa ujumbe wangu siku hizi ni ukombozi wa utumwa wa kimawazo. Kwahiyo siwezi kuendeleza uongo wa kuwa watu weusi Afrika wanaishi kwenye miti. Kucheka ni afya. Nilikuwa natania.

bado tunaishi kwenye miti?

Watoto leo asubuhi wameniuliza kama Afrika bado tunaishi kwenye miti! Hawa ni watoto ambao wangekuwa kidato cha nne hapo nyumbani. Nimewaambia kuwa ndio, tunapenda sana kulala juu ya miti na kupika huko huko. Kwahiyo kama wanataka kunitembelea Afrika lazima wajifunze kwanza kupanda juu ya miti. Na kulala pia bila kuanguka!

tutakubali hadi lini?

Ndugu yangu Mtanzania,
UTAKUBALI KUPUMBAZWA HADI LINI??

vyakula vya kisasa

Rafiki yangu Dan anasema kuwa alipotembelea Tanzania alijisikia vibaya sana. Kwanini? Alikuta kuwa watu wanadhani kuwa kuacha kula vyakula vya asili na kula vyakula vya papo kwa hapo (fast food) kama McDonalds ni moja ya alama ya maendeleo.

Matatizo ya afya yanayotokana na kula vyakula vyenye kemikali na homoni hapa Marekani yanaongezeka kila siku. Watoto wadogo wanakuwa na miili isiyoendana na umri wao. Karibu kila mtu unayekutana naye ana matatizo ya unene kupita kiasi.

Ameniuliza, hivi mfumo wenu wa elimu hauwafundishi watu wenu kuwa vyakula vyenu vya asili ni bora?

Masikini! Angejua. Mfumo wa elimu wa Tanzania???!!!! Sikuweza kumjibu maana nilikuwa nina njaa. Na kuongea juu ya "mfumo" wa elimu Tanzania inabidi uwe umeshiba.

Bob Marley ana wimbo mmoja anasema: Usikubali wakupumbaze wala wakufundishe, sisi tuna akili zetu wenyewe.
Ameimba maneno haya katika Coming From the Cold.

uandishi

Ninakwenda kufundisha watoto wa high school juu ya uandishi. Watoto wa shule hapa sio rahisi kuwafundisha. Adabu hakuna kabisa!
Baadaye.

waafrika na viongozi wao

Jana nimebishana na bwana mmoja hapa. Yeye ni Mmarekani mweupe ambaye amefika Dar Es Salaam, Zanzibar, Ghana, Afrika Kusini, na Botswana. Tumeongea masaa matatu juu ya Afrika. Hoja yake kuu ni hii: kwanini waafrika wanaawaacha viongozi wao wanauza mali asili kwa faida yao wenyewe na familia zao?

Hivi kwanini tunawaacha hawa wezi madarakani??????
Msiwaone na suti zao na sura zilizonawiri. Wezi wote hao!

6/14/2004

Umedanganywa

Hivi majuzi nilisema kuwa kuanzia sasa nitakuwa naongelea juu ya ukombozi wa akili hadi mnichoke. Mwanzo wa kufanikiwa katika jambo lolote kama taifa, kama waafrika, kama nchi masikini, ni kujikomboa toka utumwa wa kimawazo.

Narudia maneno haya niliyasema juzi: Umekuwa ukidanganywa toka uzaliwe. Mababu zako walidanganywa. Wazazi wako walidanganywa. Wewe nawe umedanganywa. Wanao utawadanganya. Dunia nzima imejaa uongo mtupu

mfumo wa elimu wa Tanzania

Ninaondoka asubuhi hii kwenda kuongea na wanafunzi ambao wanaondoka hivi karibuni kuja Afrika. Ninatakiwa kuongea nao juu ya mfumo wa elimu wa Tanzania. Sasa sijui niwaeleze juu ya shule za mbagala na maneromango au niwaeleze juu ya "academy"!

6/13/2004

kesho ni mbio

Ngoja nikalale maana kesho ni jumatatu. Mbio zinaanza. Nchi hii inajengwa kwa mbio. Hakuna muda wa kupoteza. Kesho usiku nitatazama sinema inaitwa Matrix. Nitakueleza kidogo juu ya sinema hii (ina sehemu tatu) nikishaimaliza.

Halafu jumatano ninapanga kwenda kwenye msikiti wa waislamu weusi. Hawa ni tofauti na waislamu ambao unawafahamu hapo Tanzania. Sio Sunni wala Shia. Wakati Sunni na Shia wanaamini kuwa Muhammada alikuwa nabii wa mwisho. Waislamu wa kundi la Nation of Islam wanaamini kuwa hakuwa nabii wa mwisho. Nitakupasha kidogo juu ya ziara yangu msikitini kwao.

Nitakunywa maji ya moto na asali kisha nilale.

bush na osama

Kuna sinema inatolewa mwisho wa mwezi huu. Fahrenheit 9/11 ni sinema ya Michael Moore ambayo pamoja na mambo mengine inaonyesha uhusiano wa karibu wa kibiashara na kirafiki kati ya familia ya Bush na familia ya Osama Bin Laden. Filamu hii imeshinda tuzo la tamasha la filamu la Cannes.

Sijui kama unafahamu kuwa baada ya shambulio la Septemba 11, hakuna ndege zilizoruhusiwa kuruka. Ila ndege iliyokuwa imebeba jamaa zake Osama. Hadi leo hata maofisa wa juu wa kikachero hapa Marekani wanasema hawajui amri ya kuruhusu ndege kuondoka hapa kuelekea Saudi Arabia ilitolewa na nani.

Sinema hii imetishia Hollywood. Ni hivi majuzi imeweza kupata kampuni ya kuisambaza maana kila kampuni ilikuwa ikiogopa kutia mkono. Michael Moore ana kitabu kimoja kizuri sana kinaitwa Stupid White Men

Iraki

Hakuna kiongozi yeyote hapa Marekani anayetaka kuzungumzia idadi ya wananchi wasio na hatia ambao wameshauawa hadi hivi sasa katika uvamizi wa kizandiki uliofanywa na serikali ya kidikteta ya george bush. Marekani inakwenda Iraki kutafuta silaha za sumu wakati nchi hii ina silaha za sumu ambazo zinaweza kuua dunia nyingine 100 kama hii tunayoishi!

Hivi Bush ataiba tena kura mwaka huu? Kuna kipindi kwenye luninga leo alfajiri ambacho kitakuwa na wataalamu watakaojadili jinsi Busha alivyoiba kura. Kaiba kura Marekani na sasa anaiba mafuta na rasilimali za Wairaki.

NINASOMA NINI HIVI SASA?

Ninaendelea kusoma kitabu kiitacho Smart Mobs: The Next Social Revolution. Mwandishi wa kitabu hiki, Howard Rheingold, ni kati ya watu wanaoamini kuwa zana mpya za mawasiliano kama vile mtandao wa kompyuta ni zana zinazoweza kutumiwa kuleta mabadiliko makubwa ya kijamii, kitamaduni, na kisiasa. Unaweza kufuatilia habari za "smart mob" au "flashmob" hapa: www.smartmobs.com

Kitabu hiki, kwa mfano, kinatukumbusha kuwa serikali ya Ufilipino iliangushwa kwa matumizi ya simu za mkono kutumiana ujumbe wa maneno (SMS.

gongo

Gazeti la The Guardian la Juni 14 linasema kuwa vita dhidi ya pombe ya gongo ni ngumu sana.
Kama Tanzania inashindwa kupambana na biashara ya pombe ya gongo katika jiji la Dar ambako ndio wakuu wa nchi wanaishi, je vita dhidi ya rushwa au umasikini ndio tutaiweza?

reagan

Toka aliyekuwa rais wa Marekani, Ronald Reagan, afariki redio za kihafidhina zinapiga kelele kweli. Wanadai kuwa dunia haijawahi kuwa na rais na mtu muungwana na mcha mungu kama huyu.

Jamani, jamani, jamani! Nitaandika kirefu kwenye makala yangu gazeti la Mwananchi kila jumapili juu ya Reagan.

mola tuepushe

Dakika chache zilizopita luninga moja hapa Marekani imeonyesha waandishi walioingia katika eneola jeshi lenye kemikali za sumu. Wameingia katika eneo hilo bila tabu yoyote. Wakaenda hadi kwenye mtambo mkuu wa kemikali na kisha kutoka.
Kisha wakatazama kamera na kuuliza: hivi tungekuwa magaidi?
Eneo hili ni la jeshi. Na eti kuna ulinzi. Mola atuepushe. Nchi hii imekusanya silaha za kemikali, kibaiolojia, na nyuklia. Siku wajamaa hawa wenye madevu wakivamia maeneo hayo…wala sithubutu kufikiria. Tumesikia kuwa kuna magaidi 18,000 ambao usiku na mchana wanafikiria jinsi ya kushambulia Marekani, Wamarekani, na marafiki zao.


upepe mkali usiku wa leo

Kuna mvua na upepo mkali vinakuja. Naona itabidi nilale sebuleni leo maana kuna mti mmoja mkubwa nje ya dirisha la chumba cha kulala. Kimbunga kinachokuja wanasema kinavunja miti. Silali chumbani ng’o.


Majira ya baridi ya mwaka 2002. Siku ya kwanza kuteleza kwenye theluji. Mchezo mtamu sana huu. Tena unanikumbusha enzi za utoto nilivyokuwa najitelezesha barabarani wakati wa mvua. Kulikuwa na raha yake. Tofauti ya wakati ule na sasa ni kuwa utelezi wa kule Moshi ulikuwa sio kwenye theluji bali kwenye udongo. Na sikuwa na mavazi rasmi. Nilikuwa nikitumia kisigino kuteleza!!!!!! Posted by Hello


Baba/Mama Ukweli mjini Tacoma, jimbo la washington Posted by Hello


Kila mwaka mji wa Toledo husherehekea siku ya Tanzania. Hapa nikitazama maonyesho ya kazi za sanaa toka Tanzania mwaka 2003. Mji wa Toledo ni mji dada wa mji wa Tanga. Wagosi wa Kaya oyee
 Posted by Hello

pasi na ikulu

Mwalimu mmoja wa chuo kimoja hapa Marekani kakutana nami jana. Akaniuliza, "Eti nasikia pasi imeanguka ikulu ya Tanzania na kusababisha moto. Karibu ikulu iteketee." Kisha akafumba macho na kusema, "Kweli Afrika kuna kazi nzito mbele yenu ninyi vijana."

Hili suala la ikulu kuungua sijalifuatilia kwa karibu. Sijui kama ni kweli moto ulisababishwa na pasi. Sitashangaa. Ninachoshangaa ni kuwa moto haukuteketeza ikulu maana zimamoto nchini wanafahamika kwa kwenda eneo la tukio bila maji!Wanakwenda kutazama kwanza kama kweli kuna nyumba inaungua kisha wanaondoaka kwenda kutafuta maji.

Ah, naambiwa wanafanya hivyo wanapokwenda nyumba za masikini....

mwenge wa uhuru

Hivi huu mwenge wa "uhuru" unaokimbizwa nchi nzima wakati uhuru tuliopigania tumeutoa bure kwa makampuni ya kibeberu una faida gani?

Uhuru hauletwi kwa kuwasha moto na kupoteza muda wa uzalishaji kwa kuukimbiza nchi nzima. Uhuru unapatikana kwa kuanza kukomboa fikra. Kufanya kazi. Kuwa na majadiliano ya kitaifa. Kujenga utaifa na visheni ya maendeleo. Kutokomeza utegemezi. Kujenga sekta ya sayansi na teknolojia. Kujenga mfumo wa elimu inayomkomboa mwanadamu. Kuondoa rushwa. Kujenga demokrasia ya kweli.

Lakini nadhani hii kila mtu anajua. Swali ni hili: ni vipi tutafanya mambo haya?

MFUMO WA BABILONI

Bob Marley watu wengi hatujakaa chini na kumsikiliza. Ninaweka hapo chini baadhi ya maneno katika wimbo wake wa Mfumo wa Babiloni (Babylon System). Wimbo ninaupenda sana huu. Tazama:
 
We refuse to be
What you wanted us to be
We are what we are
That's the way it's going to be, if you don't know
 
Babylon system is the vampire
Sucking the children day by day
Sucking the blood of the sufferers
Building church and university
Deceiving the people continually
Building church and university
Graduating thieves and murderers....
 
Now we know everything we got to rebel...
 


ujumbe wa leo

Najisikia kutupa bomu kanisani,
Kwani sasa unajua kuwa mhubiri anadanganya.
Nani atabaki nyumbani
Wakati wapigania uhuru wakipambana?
- Bob Marley katika wimbo wake wa Talking BLues

jumapili

Nimechelewa kulala jana usiku. Mwili umechoka kweli. Leo jumapili. Siku ya "kujifanya." Kila mtu leo anajifanya kuwa mcha mungu. Kisha kuanzia jumatatu hadi jumamosi sijui wanakuwa "wacha" kitu gani.Kila jumapil ninasikia harufu ya unafiki hewani.

Ukienda kanisani, tafadhali usisahau kupeleka kodi ya wiki: sadaka.

Nakwenda mjini kwenye msikiti wa Taifa la Waislamu (nation of islam). Yaani waislamu weusi. Ninakwenda kutafuta kanda za mahubiri ya Louis Farrakhan. Kisha nirudi nije nikapike, nile na kuketi kutazama mikanda.

Baadaye.

jumapili

Nimechelewa kulala jana usiku. Mwili umechoka kweli. Leo jumapili. Siku ya "kujifanya." Kila mtu leo anajinfanya kuwa mcha mungu. Kisha kuanzia jumatatu hadi jumamosi wanakuwa "wacha shetani."

Siku ya jumapili ni siku ninasikia harufu ya unafiki hewani. Ukienda kanisani usisahau kupeleka kodi ya wiki: sadaka.

Nakwenda mjini kwenye msikiti wa Taifa la Waislamu (nation of islam). Yaani waislamu weusi. NInakwenda kutafuta kanda za mahubiri ya Louis Farrakhan. Kisha nirudi nije nikapike, nile na kuketi kutazama mikanda.

Baadaye.

ndizi

Kesho lazima nile ndizi za kukaanga. Ndizi "Uganda" toka Karibiani. Hawa jamaa sijui wanapendea nini vyakula vyao. Vyakula vimejaa kemikali utafikiri watu wana wadudu wa kahawa mwilini mwao wanataka kuwaua!

Nimemaliza kutazama mkanda wa video wa Louis Farrakhan. Huyu ni kiongozi wa Taifa la Waislamu (Nation of Islam). Kundi la watu weusi wanaoamini kuwa uislamu ni dini ya Waafrika na kuwa nabii Eliya aliyetabiriwa kwenye biblia ni mwamerika mweusi aitwaye Elijah Muhammad, ambaye ndiye aliyejenga kundi hili. Wanaamini kuwa Elijah alikutana na mtu aitwaye Farad Muhammad ambaye alimfundisha Elijah Ukweli juu ya dunia, mungu, na wanadamu kwa miaka mitatu. Baada ya miaka mitatu Farad alitokomea.

Basi Farrakhan ni mzungumzaji hodari sana. Ana kipaji cha kuongea.

Makala yangu kwenye Mwananchi wiki mbili sasa imekuwa ikizungumzia juu ya Urasta. Nitamalizia wiki ijayo kisha nitaandika juu ya Taifa la Waislamu.

Naenda kupumzika.

UJUMBE WA LEO

Ujumbe wa Leo: Kila ujualo ni uongo.
************************************

Umekuwa ukidanganywa toka uzaliwe. Mababu zako walidanganywa. Wazazi wako walidanganywa. Wewe nawe umedanganywa. Wanao utawadanganya. Basi dunia nzima imejaa uongo mtupu.

Wimbo wa Ukombozi

Kuanzia sasa nitakuwa nazungumzia suala la ukombozi wa akili kwa nguvu zaidi. Ndio maana nimeanzisha huu ukurasa. Kwanza kabisa napenda ujue kuwa ninaamini kuwa mapinduzi ya zana mpya za mawasiliano ni mapinduzi ya kijamii, kisiasa, kiakili, na kitamaduni. Ili kuhakikisha kuwa mapinduzi haya yanakuwa na faida kwetu Watanzania. Waafrika. Lazima tuhakikishe kuwa tunaimba wimbo wa ukombozi.

Bob Marley ana wimbo unaitwa Redemption Song. Ndiko nimetoa maneno haya: wimbo wa ukombozi. Katika wimbo huo Bob analia kwa hisia, "Hautasaidia kuimba wimbo huu wa ukombozi?" Kisha anasema
"Jikomboe kutoka kwenye utumwa wa kimawazo, hakuna zaidi ya sisi wenyewe atakayeweza kukomboa akili zetu."

Kwahiyo ukija kwenye ukurasa lazima uwe tayari kukubali kufumbua macho. Kutumia uwezo uliopewa na muumba wako kufikiri na kuhoji. Hoji mamlaka. Hoji kila kitu. Jihoji hata wewe mwenyewe. Hoji. Hoji. Hoji.

****************************************************************
Da, nimechoka kweli. Saa nane usiku sasa. Lazima nikalale. Hivi nimekula? Nilishasahau. Jamani nina hamu na ugali wa kisamvu cha nazi. Jamani! mate yananitoka.
*****************************************************************

Sijaamua wiki hii nitaandika nini kwenye makala yangu ya gazeti la Mwananchi. Uwe unasoma gazeti la Mwananchi kila Jumapili. Soma makala iitwayo: Gumzo la Wiki.
****************************************************************

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com