7/08/2004

Ushamba Hotelini - 1

Siku moja, mwanzoni nilipowasili hapa, nilikwenda hotelini. Baada ya kuagiza chakula nikaenda zangu kuketi nikisubiri mhudumu aniletee. Nikasubiri. Nikasubiri. Njaa wakati huo inapiga mayowe. Mara akaniambia kuwa chakula changu kiko tayari. Nikajiuliza, "Kama kipo tayari mbona siletewi?" Nikaanza kuhisi kuwa kuna ubaguzi wa rangi. Labda huyu binti mweupe aliyeko kaunta ananichukia kutokana na rangi yangu. Nikaanza kuandaa maneno ya kumpasha. Hakuna kitu kinanchonifurahisha kama kupasha wazungu wabaguzi na kuwatazama wakishika adabu. Wakati nafikiria hivi, akaniita tena kuniambia nikachukue chakula changu. "Unasemaje?" Nikamuuliza. Yaani nimekwenda hotelini na chakula nimelipia anataka nikakibebe mwenyewe? Nikataka kupandisha. Mara nikahisi huenda kuna jambo nisiloelewa. Hivyo nikaamua kwenda kuchukua chakula changu. Lakini shingo upande. Nadhani jambo jingine lililonifanya niache kupandisha ni ukweli kuwa sijaona sehemu ambayo wahudumu wanachukuliwa kama watumwa. Watumwa ambao wanaweza kuitwa kwa namna ambayo hata mbwa akiitwa hatakwenda. Watumwa ambao wanapewa majina ya kuwadhalilisha. Watumwa ambao wakipapaswa na wateja hawana haki ya kulalamika. Wanatakiwa watabasamu. Wavute biashara. Sijaona hiyo bado. Unajua nchi hii ukicheza unajikuta jela au unalipa faini. Sheria mbele!

(KISA HIKI KITAENDELEA, RUDI TENA KUFUATILIA KILICHOTOKEA)

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com