9/21/2004

Ukiwa na Njaa Mtafuite Erick

Nimemtaja Erick kwenye makala yangu ya wiki iliyopita katika gazeti la Mwananchi. NIlikuwa nazungumzia suala la kujitolea kusaidia jamii na wanajamii. Erick hujitolea kushughulikia suala la maakuli. Ukienda kwenye tukio lolote lile la hadharani, iwe ni sinema, muziki, hotuba, maonyesho, n.k. ukakutana na Erick basi ujue kuna chakula cha bure. Kila ninapomwona lazima nicheke. Erick yeye ni mfuasi wa siasa za "kijani." Ni mtetezi wa mazingira. Anapenda sana kujitolea kusaidia. Kwa mfano, kila ijumaa lazima apike chakula kisha aende kituo kikuu cha mabasi hapa Toledo kugawa chakula hicho bure. Mpango huu wa kugawa chakula bure kituo cha basi unaitwa "Chakula, sio Mabomu" (kwa tafsiri ya kiswahili). Kawaida huwa anakwenda kwenye maduka ya vyakula vya asili (yaani visivyo na kemikali za sumu) ambako huwa anapewa chakula bure. Ikifika ijumaa anapika kisha huyoooo...kituo kikuu cha cha mabasi.

Ikitokea ukamuona Erick ukiwa na njaa, tuliza akili maana muda si mrefu utakula. Leo nilikwenda kutazama sinema ya bure iitwayo The Carlyle Connection kwenye kanisa la Central United Methodist mtaa wa Central. Sinema hii inaonyesha jinsi ambavyo familia ya Bush imekuwa na uhusiano wa muda mrefu wa kibiashara na kirafiki na familia ya Usama Bin Laden. NIlikuwa nimechelewa kidogo kwenye hiyo sinema. Nilipoingia tu nikamuona Erick ameketi. Njaa ilikuwa imenikamata kweli, lakini nilipomuona ilikuwa kama nimeshashiba. Baada ya kuketi dakika tano hivi nilinyanyuka kuelekea upande alioko Erick. Kawaida huketi au kusimama pembeni ya chakula chake. Kila anayeenda kuchukua chakula anapewa somo fupi kuhusu chakula chenyewe. "Leo hii asithubutu kuja kunipa hutba." Nilijisemea wakati nikielekea kwenye meza iliyoshehena vyakula vya nguvu.

Baada ya kula na kushiba vilivyo, Erick alinijia, "Ukitaka chakula zaidi unaweza kuchukua upeleke nyumbani." Huyu ndio Erick mwenyewe. Lazima ukishakula akushawishi uchukue chakula nyumbani.

Huyo ni Erick. Nikimtazama simmalizi. Sijui muda wa kupika vyakula vyote hivi kila kukiwa na tukio anapata wapi. Pamoja na kuwa ni mwanafunzi, Erick akizuka kwenye tukio lolote lazima awe na mikoba ya chakula. Imefika wakati ukiongea naye unaona kama vile unaongea na hoteli.

Erick na chakula chake. Kuna wakati nikimwaza nikiwa peke yangu ninabaki kucheka. Sio muongeaji sana. Anapenda kutazama huku akitabasamu. Akiongea itakuwa kuhusu chakula!
Jambo la ajabu ni kuwa sijawahi kumuona Erick akila!!

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com