12/28/2004

KWANINI KAZI HAZIPATIKANI BONGOLAND?

Niliipata barua pepe iliyonipa jibu la swali hilo hapo juu zamani kidogo. Nikaibandika pembeni ya meza yangu. Kila mara nikawa nikiisoma na kuitafakari. Ni barua pepe ambayo imekuwa ikizunguka kwa muda kwenye mtandao. Huenda uliwahi kuipata. Siwezi kujua mwandishi wake hasa ni nani. Ila ninachojua ni kuwa kilichomo ndani yake sio mzaha. Ukiisoma unaweza ucheke. Hakuna ubaya. Ila tafakari undani wake.

Ninajiuliza maswali haya kila mara: Ni lini Tanzania itaachwa kuitwa nchi masikini? Ni lini Tanzania itaacha kuwa nchi
inayoendelea na kuwa nchi iliyoendelea? Hivi hiyo siku itakaa ije?

Kuna wakati huwa ninasita kusema kuwa Tanzania ni nchi inayoendelea. Kuendelea sio neno tu. Kuendelea ni hali ambayo unaweza kuipima. Karibu kila kipimo cha maendeleo ukikitumia, unaona kuwa Tanzania inarudi nyuma badala ya kwenda mbele. Kwa mfano siku zinavyokwenda wastani wa umri wa Mtanzania kuishi hapa duniani unapungua. Yaani kama wewe ni mtanzania unayeishi Tanzania, mauti utaikaribia kwa haraka sana! Najua inatisha, nisiseme?

Kwahiyo utaona ingawa inachukuliwa kuwa mataifa hapa duniani yamegawanyika kati ya yale
yanayoendelea na yaliyoendelea, ukweli ni kuwa kuna mataifa mengine yasiyoendelea, yaliyosimama na yanayorudi nyuma!

Haya, turudi kwenye swali la msingi. Kwanini ajira ni vigumu kupatikana Bongoland? Isome barua pepe ninayoizungumzia upate jibu la kwanini hakuna ajira Tanzania:
George Chege amepunguzwa kazi hivi karibuni. Amepania kutafuta kazi nyingine kwa udi na uvumba. Ameamshwa asubuhi ya leo na mlio wa saa ya mezani. Ni saa 12 alfajiri. Saa yake ya mezani imetengenezwa nchi Japani. Anaamka na kuweka maji ya chai katika jiko lililotengenezwa China huku akinyoa ndevu zake kwa mashine ya kunyolea iliyotengenezwa Hong Kong.

Anapomaliza kuoga kwa sabuni iliyotengenezwa Kenya, anavaa shati lililotengenezwa Uingereza na suruali ya dengirizi iliyotengenezwa Marekani na viatu vya Kimarekani vilivyotengenezwa na wafanyakazi wa ujira mdogo huko Vietnam. Anakunywa chai kwenye meza iliyoagizwa toka Dubai na kula mayai yaliyokaangwa katika kikaangio kilichotengenezwa India. Sahani, kijiko na kikombe anavyotumia vimetoka China.

Anafungua redio yake kisasa iliyotengenezwa Taiwan huku akifungua kitabu chake cha kumbukumbu kilichotengenezwa Italia ili aweze kupanga ratiba yake ya siku kwa kalamu toka Uingereza.

Anapomaliza kupanga ratiba yake ananyanyua simu yake ya mkononi toka Japan na kuondoka kuelekea kwenye kituo cha basi ambako anapakia basi lililotengenezwa Japan na kununuliwa Dubai.

Jioni inapowadia anarudi nyumbani akiwa mchovu kabisa. Anaketi kwenye viti vilivyotengenezwa Singapore na kuanza kutazama kipindi cha luninga kilichotayarishwa Marekani kwenye luninga iliyotengenezwa Taiwan. Wakati akitazama luninga anajiuliza sababu inayofanya iwe vigumu kwake kupata kazi. Haelewi.
** (Usisahau kuwa hata jina lake, George, limeagizwa toka Ulaya).

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com