2/12/2005

BWANA UKWELI

Bwana Ukweli kaanza kutumia "cha" kama kwenye , 'kiti cha Ukweli.' Ambacho hajajua ni kuwa husemi "cha" kwa kila kitu. Kwa mfano anavyosema, "Mpira cha Ukweli." Au alivyosema leo asubuhi, "Kofia cha Ukweli."

Umri?
Anakaribia miwili na nusu.
Anaongea lugha ngapi? Tatu!
Tatu?
Ndio, tatu. Ya kwanza alianza nadhani akiwa na miezi sita au saba. Wakati huo alianza kujifunza lugha ya ishara kama wanayotumia viziwi. Ufundishaji wa watoto lugha ya ishara unaanza kuenea kwa kasi. Wanasaikolojia walitafiti wakagundua kuwa tunapoacha watoto waishi kwa miaka kadhaa kabla hawajaweza kuwasiliana nasi zaidi ya kulia ni kama mateso.

Watu wazima tunashindwa kujizuia hata tukiwa tumekutana na watu tusiowajua. Yanayotokea ndani ya mabasi unajua. Mwanzoni mkaa kimya kama vile hamjui kuongea, lakini wakati wote huo kuna kisu kinawakata ndani kwa ndani, mnataka kuongea na kumjua mwingine. Hiyo ni kiu ya kuwasiliana.

Mtoto mchanga haina maana hana mambo anayotaka kukwambia. Anayo mambo mengi ila mfumo unaotumiwa kukueleza jambo inabidi ajifunze kwa muda mrefu zaidi. Hapo ndio unaona mtoto akitaka kitu analia. Mzazi anaanza kutumia "utabiri" kujua mtoto anataka nini.

Kulia kwa mtoto wakati mwingine sio kwamba anataka kitu bali kuna jambo anataka kukwambia ila anashindwa. Kulia kunakuwa ni njia ya kupambana na kuchanganyikiwa. Fikiria wakati mwingine unapopata hasira unapomwambia mtu kitu lakini hakusikii. Mtoto naye anaposhindwa namna ya kukwambia anapata ghadhabu.

Kwahiyo watoto wanafundishwa jinsi ya kutumia alama za mikono. Uwezo wao wa kutumia mikono wakati huu uko juu zaidi ya uwezo wa kutumia sauti na kuunda maneno.

Mwanzoni nilifikiri kuwa hii ni porojo. Mtoto atumie alama za vidole na viganja? Nilijiuliza nikiwa ninasita kuamini kwa haraka. Baada ya Mama Ukweli kumpatia Bwana Ukweli shule ya matumizi ya ishara kuongea nilishuhudia mwenyewe. Bwana Ukweli alianza kujua kusema, "Naomba kunyonya," "Naomba maji," "Nataka kulala." "Acha," "Miti," "Ndege," "Asante,"
"Zaidi," n.k.

Sikumbuki kule juu nilianza na kitu gani. Na kwakuwa nimechoka sana, siwezi kurudia kusoma. Ninaishia hapa. Ninywe maji ya moto nilale. UWE UNAKUNYWA MAJI YA MOTO KABLA YA KULALA.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com