2/23/2005

NANI ANAFAA KUWA RAIS WA TANZANIA?

Nimeulizwa hili swali mara elfeni: Ndesanjo, unadhani nani anafaa kuwa rais wa Tanzania?
Nina majibu kadhaa ya swali hili.
Jibu la kwanza: Kwakuwa Watanzania wengi wanajifanya kuwa ni waumini wa dini hizi mbili za kuja, uislamu na ukristo, naona basi tuwe na marais wawili. Tuwe na shehe mkuu na askofu mkuu maana watu hawa inadaiwa kuwa wanaongozwa na mungu. Nani zaidi ya watumishi wa mungu wenye mawasiliano ya moja kwa moja na mungu wanaoweza kuongoza taifa ambalo linaweza kuelezewa kuwa ni sawa na merikebu isiyo na nahodha? Kwahiyo tuwe na hawa "watumishi" wa mungu kama marais wetu maana kwa maneno mengine, mungu wa ukristo na uislamu ndiye atakuwa rais wetu. Sina uhakika kama mungu wa dini hizi mbili za kuja ni mmoja au ni wawili tofauti, tusije tukawa kama tuna marais wawili! Nadhani dini hizi mbili zina miungu tofauti maana mungu wa dini moja anasema kula nguruwe ni sawa, na wa dini nyingine anasema sio sawa. Mungu wa dini hii anasema kuwa Yeshua/Isa (Yesu) alisulubiwa, wa dini nyingine anasema hakusukulubiwa. Wa dini hii anasema kuna kitu kinaitwa utatu na mungu wa dini nyingine ambaye hajui kichagga au kisukuma bali kiarabu anasema kuwa hakuna utatu...dhana ya utatu ni shirk. Mungu wa dini hii anasema kuwa biblia ndio kitabu chenye ujumbe wake, na wa dini hii anasema maneno yake yako kwenye zaburi, torati, manabii, injili, na kurani! Nadhani hawa ni miungu wawili tofauti. Kama sio, basi atakuwa anasahausahau sana!
Narudi kwenye urais Tanzania:
Hili ni jibu la pili kuhusu nani anafaa kuwa rais wa nchi yetu (kama bado tuna nchi!): Naona ili "tuendelee" kama wenzetu waliokuja zamani na kutupa biblia kisha wakatuambia tufumbe macho kusali, na tulipofumbua tukakuta tumebaki na biblia na wao wamechukua ardhi, maliasili, ndugu zetu (watumwa) na nafsi zetu... na ili kuendana na mtazamo kuwa ubinafsishaji ndio njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na HURU, tubinafsishe kiti cha urais! Kwa kuwa tunabinafsisha viwanda, migodi, mabenki, mashamba, n.k kwa kuwa tumeshindwa kuendesha wenyewe, kwanini tusibinafsishe ikulu kutokana na ukweli kuwa tumeshindwa kuendesha nchi yetu?
Ndio, tuzunguke huku na huko kwa wazungu, kutafuta mzungu atakayeshinda tenda ya kuwa mnyapara wetu. Tutakachofanya ni kumpaka masizi ili ngozi yake ifanane na sisi kama walivyo watawala wetu wanaoitwa "viongozi" ambao ngozi zao ni kama zetu ila akili na nafsi zao sio. Wananikumbusha kitabu cha Frantz Fanon cha Black Skin, White Mask.
Aah, kuna jibu la tatu ambalo limenijia akilini sasa hivi: Kwanini tusimwombe rais Joji Kichaka wa Marekani ambaye pia ni rais wa Afghanistani na Iraki aongeze Tanzania katika nchi anazoongoza??????
Nyie mnasemaje?

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com