2/12/2005

SUMAYE ACHA KUTANIA!

Nasikia kuwa Sumaye, yaani Waziri Mkuu wa Tanzania, ametangaza rasmi kuwa anataka kugombea urais. Niliwahi kuandika ndani ya blogu hii kuhusu madai kuwa Sumaye ana nia kama hiyo. Nilisema kuwa watu wanamsingizia maana ninaamini kuwa anajua fika kuwa hawezi kabisa kazi hii. Kama kazi ya Uwaziri Mkuu ameshindwa, atawezaje Urais?

Kumbe nilikuwa ninaota. Sasa ametamka kuwa anataka urais. Anataka kukimbilia kule Mwalimu Nyerere alikowahi kuwauliza, "Kuna nini, mbona mnakimbilia huko?"

Hoja yangu kuu niliyoitoa nikisema kuwa Sumaye hawezi urais ilikuwa ni hii: Tanzania inapitia kipindi kigumu sana cha mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kitamaduni, na kisiasa. Kipindi hiki kimevaa shati la rushwa, suruali ya ubadhirifu, na viatu vya mikataba ya kitapeli. Kwa misingi hiyo tunahitaji viongozi wenye kuwa na njozi. Vingozi wenye visheni. Viongozi ambao wana uwezo wa kuongoza zaidi ya kuhutubia na kuzunguka huku na huko kuzindua kitu wanaita, "miradi ya maendeleo."

Tazama Tanzania: barabara toka enzi za mkoloni mpaka leo. Kilimo tumeshindwa huku tumebaki na wimbo wa "kilimo uti wa mgongo wa taifa." Nadhani wanachosema katika wimbo huu ni kuwa kilimo ni ugonjwa wa uti wa mgongo wa taifa. Neno ugonjwa huwa wanalisema kimya kimya.

Biashara tumeshindwa. Viwanda tumeua. Elimu bado tunayo ile ya mtu kujua kusoma na kuandika. Kwenye afya, wanawake wanazalia sakafuni, wengine nje ya hospitali. Migodi tumeshindwa kuendesha. Utalii wakenya wametunzunguka hadi mlima kilimanjaro umekuwa wa kwao!

Rafiki yangu mmoja kaniambia kuwa wageni wakishachuma maliasili, utafika wakati hata funza hawaitaka Tanzania.

Tembelea tovuti hii ya ofisi ya Sumaye. Kwanza tazama lugha gani imetumika. Kisha ukikutana na Sumaye muulize anapohutubia wananchi huko Newala, Bariadi, Lushoto, Babati, n.k. huwa anatumia lugha gani? Kama anatumia Kiswahili, kwanini tovuti yake imejaa kimombo cha kule kwa Malikia Lizabeti? Kisha mdhihaki kidogo, mwambie kuanzia sasa aanze kuzunguka nchi nzima akihutubia kwa kiingereza! (Nimeandika gumzo la wiki juu ya suala hili, ambayo nitaiweka ikishachapishwa kule Tanzania).

Ukishafika kwenye tovuti hiyo tazama picha yake akijifanya yuko "bize." Kila nikimwangalia ninajiuliza, "Hivi ni mkataba gani wa ulaghai alikuwa anasaini alipopiga hiyo picha?" Hawa watu wananitisha sana ninapowaona na suti zao na kalamu za gharama wakitia wino mikataba. Inanikumbusha Mangungo wa Msovero!
Nenda hapa.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com