3/28/2005

MASAHIBU YA WALIMU NA ELIMU TANZANIA

Kuna habari katika inayosikitisha sana kuhusu walimu na elimu nchini Tanzania. Mengi yaliyosemwa katika habari hii sio mapya. Ninafahamiana na walimu wengi, marafiki na ndugu. Ninajua mtazamo wa sirikali ya Tanzania katika masuala ya elimu kwa wote. Kama tunataka nchi yetu iondoke katika orodha ya nchi fukara zisizo na mbele wala nyuma duniani lazima turekebishe mfumo wa elimu na kuwapa walimu heshima zaidi na kuwapa ujira halali kwa kazi kubwa wanayofanya. Soma habari yenyewe hapa. Unaweza pia kutembelea tovuti ya shirika lisilo la kisirikali, HakiElimu, linalojihusisha na masuala ya sera na mfumo wa elimu Tanzania. Hapa. Taarifa nilizonazo ni kuwa kazi ya shirika hili inahitaji pongezi. Nawapa pongezi zangu. Lakini sitaacha kuzungumzia suala hili: utaona kuwa tovuti yao ina tatizo lile ninalozungumzia kila kukicha. Wakati dhumuni kubwa la Hakielimu ni kuhimiza ushirikishwaji wa umma katika uendeshaji wa sekta ya elimu, tovuti yao ni ya kiingereza. Lugha inayotumiwa kila siku na huo "umma" katika mabasi, baa, makanisani na misikitini, majumbani, ndotoni, mikutano ya hadhara ya kisiasa, vijiweni, n.k. ni Kiswahili. Sijui kuna ugumu gani wa wanaharakati wetu kuelewa jambo hili rahisi namna hii: Watanzania wanaelewa Kiswahili zaidi ya kiingereza. Kwisha! Sisemi kuwa kiingereza ni lugha isiyofaa, hata kidogo. Hii ni lugha tunaweza kutumia tunapokuwa na maingiliano na wengine wasiojua Kiswahili. Ila tunapokuwa tunaongea sisi kwa sisi, kuna ugumu gani wa kutumia Kiswahili? Kuna hoja kuwa lugha ya kiingereza inatumiwa katika tovuti nyingi Tanzania (kama ya bunge, ikulu, ofisi ya waziri mkuu, KKKT, n.k.) maana watu wanaotumia teknolojia ya mtandao wa tarakilishi (intaneti) wengi ni wasomi wanaojua kiingereza. Hii ni sawa na kusema kuwa kwakuwa Wafaransa wengi wanaotumia mtandao wa tarakilishi wanajua kiingereza, kwahiyo tovuti ya serikali na bunge la Ufaransa na kila kitu nchini humo viwe kwa lugha ya kiingereza! Hoja hii (ya kuwa Watanzania wanaotumia mtandao huu wanajua kiingereza ndio maana tovuti ni za kiingereza) tuiweke kiporo kwa sasa, nitaikabili kichwa kichwa hivi karibuni.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com