4/28/2005

WAZEE AFRIKA NI VYUO VIKUU!

Wazee Afrika ni vyuo vikuu ni moja ya makala mpya nne nilizoweka hapa bloguni leo. Nilikuwa sijapandisha makala zangu kwa muda. Sasa nimeweka nne kwa wakati mmoja. Makala zote hizi tayari zimetoka kwenye safu yangu ya kila jumapili, Gumzo la Wiki, katika gazeti la Mwanchi nchini Tanzania. Makala zenyewe ni hizi (bonyeza juu ya kichwa cha makala unayotaka kusoma): 1. Wazee Afrika ni yuo Vikuu 2. Wamasai, Polisi, Watumishi, na Watumikiwa 3. Ukoloni Mpya Umejificha: Jiandae kifikra 4. Mapana na Marefu ya Neno Amani
Makala hizi na nyingine ziko katika kona ya makala zangu upande wa kuume wa blogu, chini ya picha yangu.

MAJINA YA MUNGU YA KIAFRIKA

Kwa wale wanaomjua mungu kwa jina lake ni Allah au Yehova tu, nenda hapa.

MKUTANO WA "BlogHer"

Kama sio Mama Junkyard pengine nisingefuatilia suala la kublogu toka kwenye mkutano wa wanablogu wanawake, BlogHer. Kutokana na juhudi na taarifa toka kwa Mama Junkyard kuna uwezekano mkubwa nikaenda kublogu moja kwa moja kwa lugha ya Kiswahili toka katika mkutano huo hapo majaaliwa ya Ruwa, mwezi wa saba.

HABARI MBALIMBALI KUHUSU BLOGU

Fuata kiungo hiki hapa usome habari mbalimbali kwa kiingereza kuhusu teknolojia ya blogu.

4/26/2005

KWA WATUNZI WA VITABU

Kama wewe ni mtunzi wa vitabu na hutaki kupigapiga hodi kwa wachapaji au huna fedha za kuchapa kitabu chako mwenyewe, teknolojia ya uchapaji mtandaoni inakuwezesha kuchapa kitabu chako bure. Unabisha? Nenda hapa.

TOGO: FAMILIA INAENDELEA KUPORA NCHI

Mtoto wa aliyekuwa mwizi mkuu wa nchi ya Togo kwa karibu miaka 40, Faure Gnassingbe, amehalalishwa kuendelea kazi ya wizi aliyoianza baba yake miongo mingi iliyopita. Soma hapa.

BLOGU YA ALIYEKUWA WAZIRI MKUU WA USWIDI

Hii hapa ni blogu ya aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Uswidi.

4/25/2005

PAPA ANGETOKEA AFRIKA?

Kabla papa mpya kuchaguliwa na wanadamu (ni wanadamu wanapiga kura kuchagua papa na sio mungu), baadhi ya wasomaji walikuwa wananiuliza kama nilikuwa naunga mkono suala la papa mpya kutokea Afrika. Nilishindwa kuwajibu. Sifahamu kwanini waliniuliza swali namba mbili kabla hawajaniuliza swali namba moja. Wangeniuliza kwanza kama ninaunga mkono kuwepo kwa cheo cha upapa hapa duniani. Au kama ninajali kuwepo kwa cheo hicho. Au kuwepo kwa kanisa katoliki la kirumi kabisa.
Nini kitafanya nijali kuwepo kwa kanisa hili la kirumi lililodanganya watu wangu wakaacha imani zao? Labda siku wakiondoa herufi "R" kwenye RC, yaani Roman Catholic na kuweka herufi "A" ili kuwa na AC, yaani African Catholic. Hebu niache kupoteza muda, kwanza hata hiyo African Catholic ya nini?
Hivi papa angetokea Afrika, angehamia Afrika na kuanza kunywa mvinyo wa asili kama mbege badala ya mvinyo toka magharibi? Kuna rafiki yangu mhubiri ambaye hivi karibuni ataanza kutoa mbege kila jumapili kama damu ya yesu iliyomwagika msalabani kwa dhambi za wanadamu. Ingawa habari yote hii ya damu kumwagika najua ni riwaya fulani, kitendo cha kutumia mbege kinanifanya nitake kuingia kanisa lake. Mchungaji anamhimiza muumini, "Ria se kidogo kwa jina la Bwana!"

4/24/2005

MZUNGUKO WA MAARIFA YA WANADAMU

Tazama filamu ya jamaa wa Creative Commons (Afrika Kusini) inayohusu mzunguko wa maarifa. Iko Hapa.

KENYA: WATUMIA SIMU ZA MKONO KUTAFUTIA KAZI

Kule Kenya wenye simu za mkono wanaweza kutafuta kazi kwa kutumia huduma ya ujumbe wa maandishi. Bonyeza hapa.

RUSHWA KATIKA NCHI ZA KIBEPARI

Wengi wetu huamini kuwa rushwa iko katika nchi zinazoitwa changa kama vile Tanzania. Jambo tusilojua ni kuwa rushwa katika nchi za kibepari imejificha sana. Mara chache hutokea watu wakang'amua kama ambavyo imetokea hivi karibuni ambapo mla rushwa katika chama cha Republican anaandamwa kwa mambo yake kuwekwa hadharani. Kila anapojitokeza kukanusha hili, jingine linatoka kesho yake. Sijui ni lini atanyanyua mkono na kukubali. Hebu soma habari hii.

MAPINDUZI KILA KONA....

Mapinduzi ya kila aina yanatokea kila upande. Wananchi walichachamaa na kuandamana (kule Jojia, Ukraine, Lebanoni serikali zikaanguka. Sasa huko Ecuador nako maandamano ya umma yameangusha serikali. Soma hapa, hapa , hapa na hapa. Wapi kunafuatia? Zimbabwe? Kenya? Tanzania? Marekani?

BLOGU YA KI-SHONA

Polepole ndio mwendo, walituambia wahenga. Blogu za lugha za Kiafrika zinaongezeka kadri siku zinavyokwenda. Ukiacha blogu za Kiswahili, kuna blogu moja ya Ki-Bambara (Mali) ambayo bado ninatafuta anuani yake. Halafu kuna blogu nyingine ya rafiki yangu, Mokhtar, inakuja kwa lugha ya Ki-Berber. Kuna blogu ya Ki-Shona. Bonyeza hapa.

UNATAKA KUANDIKIANA BARUAPEPE NA PAPA MPYA?

Dalili za kuwa dunia imeingia kwenye mapinduzi ya zana mpya za mawasiliano ni nyingi. Ila mojawapo ni hii: papa mpya wa dini ya kikatoliki ya Roma ana anuani ya barua pepe. Kama unataka kuandikiana naye, mwandikie kwa anuani hii: benedettoxvi@vatican.va

UVAMIZI WA USIKU

Msomaji wangu wa siku nyingi, Patrick Mwasomola, kaandika dakika chache zilizopita kwenye kitabu cha wageni. Anatukumbusha maneno ya unabii ya Bob Marley katika wimbo wake wa Uvamizi wa Usiku (Ambush In the Night). Hivi ndivyo alivyoandika:

Nimemkumbuka Bob Marley leo anatukumbusha kuwa:
WAMEKUWA WAKITULAGHAI
KWA SPEA PATI, PESA, NA BUNDUKI ZAO...
*****************************************

Katika wimbo huo Bob alikuwa akizungumzia mabepari ambao leo hii tunawaita wawekezaji na wahisani. Kama una rekodi ya Bob kasikilize wimbo huo vizuri.
** Neno jingine la kiswahili la Spea Pati ni Vipuli.

4/20/2005

KUMEKUCHA!! BLOGU NILIYOKUWA NIKIISUBIRI IMEKUJA...

Nilipanga kublogu habari hii leo asubuhi lakini kwa kuwa asubuhi la leo lakini kutokana na sababu za kiufundi nilishindwa. Ninadiriki kusema kuwa katika ulimwengu wa blogu za Kiswahili ndio kumekucha sasa. Blogu niliyokuwa niliyokuwa nikiisubiri kwa muda mrefu sana imejitokeza toka matawi ya chini huko Australia. Hii ni blogu iitwayo Mwandani ya Joseph Nambiza Tungaraza, Mtanzania anayeishi nchini Australia. Hivi ndivyo anavyosema mwenyewe juu ya blogu hiyo: Mwandani keshaingia ulimwengu wa blogu.Humu ndani ya blogu hii nitapeperusha mawazo kadiri yanavyovinjari kichwani – siasa, utamaduni, sanaa, mapenzi, ubinadamu, mahusiano ya watu wa rangi tofauti, matabaka tofauti, mataifa tofauti - kadhalika maswala ya haki na demokrasia yetu Waafrika.

Ukienda katika blogu hiyo utakutana na mjadala mfupi kuhusu kifo cha Papa Yohane Paulo. Nimependa sana hoja anazojadili. Nimependa kwa mfano pale anaposema kuwa kama uchaguzi wa Papa ni uchaguzi wa mwakilishi wa Mungu duniani, hakuna haja ya watu kutaka eti Papa atoke sijui Afrika au Marekani ya Kusini. Ninakubaliana naye kabisa maana kwa mungu sisi wote ni familia moja. Hakuna masuala ya rangi au jiografia. Haya, tembelea blogu ya Mwandani (au tuseme mtembelee Tungaraza) hapa.

UNAMFAHAMU ETHAN ZUCKERMAN

Juzi jumapili nilikutana na mmoja wa watu ambao nimekuwa nikiwafuatilia kwa muda mrefu toka nianze kujiingiza katika masuala ya blogu na teknolojia mpya za mawasiliano na habari, Ethan Zuckerman. Tulikutana katika mgahawa huu hapa. Tulizungumza juu ya mambo mbalimbali kuhusu blogu za Kiswahili na mradi anaoendesha wa Global Voices. Ni siku nyingi sana toka nikutane ana kwa ana na mtu anayeelewa kwa undani masuala ya teknolojia na pia siasa na tamaduni za Afrika na nchi nyingine duniani.
Nitaongelea kwa undani mazungumzo yetu baadaye. Kwa sasa ningependa umfahamu Zuckerman. Ethan Zuckerman ni mtafiti katika chuo kikuu cha Harvard. Habari zaidi juu yake hapo Harvard na mengine ambayo amewahi kufanya hapa. Soma blogu yake hapa. Pia kuna mahojiano yake hapa. Anajihusisha na mradi wa world changing. Kongoli hapa. Na mkono wake uko nyuma ya mradi huu hapa.



4/18/2005

SIKILIZA REDIO YA MTANDAONI: JAMBO RADIO

Nimekutana na hii redio ya mtandaoni wakati nikitembelea tovuti ya www.uchaguzitanzania.com. Hivi sasa ninawasikiliza washairi wa mijini (huku ughaibuni wanawaita "urban poets") wakishusha aya bin aya. Sijui jamaa hawa ni akina nani. Ila jamaa wanaandika mashairi sio mchezo. Nadhani huyu ni Juma Nature. Tembelea redio hii hapa.

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU TANZANIA

Moja ya mabadiliko makubwa yanayotokana na teknolojia ya zana mpya za habari za mawasiliano na habari ni uwezo wa wananchi wenye nyenzo hizi kuweza kupata habari kwa urahisi zaidi na pia kushiriki katika mijadala ya kisiasa. Mfano mmojawapo ni tovuti ya uchaguzi Tanzania iliyoko hapa.

MAKALA MPYA MBILI ZA PADRI KARUGENDO

Kuna makala mpya mbili motomoto za Padri Karugendo. Ya kwanza inazumguzia mjadala ulioendeshwa na Tido Mhando wa BBC na Profesa Chachage na Mama Luhane kuhusu Papa Paulo. Kichwa chake ni: Papa Yohane Paulo: Hasi na Chanya. Isome hapa. Nyingine inauliza juu ya ukimya wa upinzani kipindi hiki ambacho moto wa uchaguzi mkuu tayari umewashwa. Isome hapa. Makala zake nyingine ziko kwenye kona yake, Kalamu ya Padri Karugendo chini ya makala zangu na Freddy Macha. Sijapandisha makala zangu muda kidogo. Nitafanya hivyo leo. Pia baadhi mmeniuliza mbona nimekuwa kimya kuhusu kifo cha Papa Paulo. Nadhani nimetaka nyoyo za watu zitulie kwanza kabla sijasema lolote.

PADRI KARUGENDO AMJIBU KHALID S. MTWANGI

Padri Karugendo aliandika makala iitwayo Yu Wapi Desmond Tutu wa Tanzania? Makala hiyo ambayo nilishaiweka katika kona ya makala zake iko hapa. Ndugu Khalid S. Mtwangi akamjibu Padri Karugendo. Niliweka jibu lake katika kona ya Karugendo. Unaweza kusoma jibu la Mtwangi hapa. Padri Karugendo naye kamjibu ndugu Khalid Mtwangi. Jibu lake hili hapa. Nimeliweka pia kwenye kona yake, Kalamu ya Karugendo, kwahiyo unaweza kusoma jibu lake wakati wowote.

4/17/2005

MKUTANO WA AFROGEEKS 2005

Ratiba ya ule mkutano unaonifanya nijichimbie imetolewa. Mada yangu nitaitoa siku ya jumamosi, Mei 21, saa saba na nusu hadi tisa kasorobo. Nitashiriki katika jopo na washiriki wengine wawili. Mmoja ni huyu, na mwingine ni huyu. Mratibu wa mjadala atakuwa ni Bruce Bimber. Mtazame hapa.
Hii hapa ndio ratiba ya jopo nitakaloshiriki:
1:30-2:45
Panel: Geek Speak: Decipherin’ Digital Heiroglyphs
Moderator: Bruce Bimber
Ndesanjo Macha "Decolonizing the African Blogsphere: The Case of Kiswahili"
Jarita C. Holbrook "Cultural Astronomy, Black Physicists, and Total Solar Eclipses"
Skip Ellis "Project NEEM: Technology for Enhancement of Distributed Meetings"

Kwa ratiba nzima ya mkutano huo nenda hapa.

MWANA BLOGU WA KWANZA WA KIKE WA KISWAHILI!!!

Hayawi, hayawi, yamekuwa! Hatimaye mwanablogu mwanamke wa kwanza wa Kiswahili duniani amebisha hodi kwenye ulimwengu wa blogu. Nasi tunaitikia: Karibu mwanamama, binti Afrika!
Kwa muda mrefu nimekuwa nikijiuliza, ni lini atatokea mwanamke mwanablogu toka Tanzania? Sauti ya wanawake toka Tanzania inahitajika kwenye ulimwengu wa blogu kwakuwa sauti hiyo imekandamizwa kwa muda mrefu na kudhihakiwa katika vyombo vikubwa vya habari. Mwanablogu huyo anayeandika historia anaitwa Zainab Yusuph. Anasema: Dunia sio mbaya, walimwengu ndio wana visa! Katika ukurasa wa maelezo yake binafsi anatuambia: Mkombozi wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe. Tembelea blogu yake hapa.
Kwa ujumla hivi sasa kuna blogu kumi za Kiswahili. Kenda toka Tanzania na moja toka Kenya. Ipo nyingine ya kumi na moja ambayo bado mwanablogu mwenyewe hajapenda iwekwe hadharani. Polepole ndio mwendo, walisema wahenga. Ukitaka kutembelea blogu hizo nenda kwenye kona ya viunganishi vya blogu za Kiswahili, upande wa kuume wa blogu hii (chini ya maelezo binafsi na makala mbalimbali).

4/15/2005

PODIKASITI NA MAZISHI YA PAPA

Ingawa nimebanwa nimeona niwamegee habari hii ya mapinduzi ya teknolojia ya habari. Hapa. Habari zaidi juu ya teknolojia ya kupodikasiti hapa. Pia nina makala ya Karugendo ambayo ni jibu kwa changamoto aliyopewa na mmoja wa wasomaji wake. Baadaye. Nawatakieni kila la kheri katika yote mnayofanya. Uhuru Daima!

4/13/2005

BLOGU NYINGINE YA KISWAHILI HIYOOO!

Kuna mwanablogu mpya wa Kiswahili, Egidio Ndabagoye, toka Moshi, Tanzania. Katika blogu yake anasema: Wanaozungumza hawajui, wanaojua hawazungumzi! Pia anatukumbusha kuwa Edward Moringe Sokoine alifariki tarehe 12 mwezi wa nne. Anauliza kama kuna anayemkumbuka. Blogu za Kiswahili zinaongezeka polepole. Moja baada ya nyingine. Polepole ndio mwendo. Mwenda pole hajikwai, akijikwaa haanguki, akianguka haumii. Haraka haraka haina baraka. Kidogo kidogo hujaza kibaba...mababu walitufunza. Mtembelee mwanablogu huyu hapa.

4/11/2005

MAKALA ZA PADRI KARUGENDO HIZOOOOO....

Nimeweka makala tano mpya za Padri Karugendo katika kona yake hapa bloguni iitwayo Kalamu ya Padri Karugendo. Kona yake iko upande wa kuume, chini ya makala zangu na za Freddy Macha. Nitaziweka makala hizo hapa, ila unaweza kuzisoma wakati wowote (hizi mpya na nyingine za nyuma) katika hiyo kona yake. Nimeweka pia makala moja katika kona hiyo, ambayo haijaandikwa na Padri Karugendo. Makala hiyo imeandikwa na ndugu Khalid S. Mtwangi. Yeye alikuwa akijibu makala ya Karugendo isemayo yu wapi Desmond Tutu wa Tanzania. Makala zenyewe ni hizi: 1. Buriani kwa Papa Paulo, hapa. 2.Mangula Ana Maana Gani? Hapa. 3. Nyamwasi wa Chuo Kikuu Dasalama, hapa. 4. Mtoto wa Mkapa na Harusi ya Kifahari, hapa. 5. Vyombo vya Habari, Utamaduni na Mila za Kiafrika, hapa. Makala ya Khalid Mtwangi iko hapa. Makala hii ni jibu kwa makala hii hapa ya Padri Karugendo. Nipatapo nafasi mwezi ujao nitajaribu kujibu baadhi ya hoja alizotoa bwana Mtwangi. Nadhani mjadala huu ni mzuri sana. Unafaa kuendelezwa, kupanuliwa, na kurefushwa.

4/10/2005

MAKALA NA HADITHI TOKA KWA FREDDY MACHA

Nimeweka makala mpya na hadithi toka Uingereza kwa Freddy Macha. Kuna hadithi aliyoiandika mwaka 1976 pale Buguruni, jijini Dasalama iitwayo Balaa! Bonyeza hapa uisome. Pia kuna makala aliyoandika kuhusu mwanamuziki mahiri wa Tanzania King Kiki wakati alipotembelea Uingereza. Isome hapa. Kingi Kiki ndiye aliyeimba, "Mimi msafiri bado nipo njia, sijui lini nitafika. Ninaulizia kule ninakokwenda..." Halafu kuna makala (sehemu ya kwanza hadi ya tatu) kuhusu umuhimu wa wanawake kujifunza sanaa ya kujilinda (martial arts). Zisome hapa, hapa, na hapa. Usisahau kuwa makala zake nyingine ziko katika kona yake hapa ndani blogu. Zitazame upande wa kuume wa blogu hii chini ya makala zangu.

NENO "PASSWORD" KWA KISWAHILI

Password = Nywila (neno nywila limetokana na neno nywilanywila ambalo lilikuwa ni neno la siri wakati wa vita vya kumwondoa mkoloni wa kijerumani nchini Tanzania. Vita hivyo ni vile vya Majimaji vya mwaka 1904-05 vilivyoongozwa na Kinjeketile Ngwale.

4/08/2005

SAMAHANINI KUHUSU MAKALA ZA PADRI NA FREDDY

Ninawaomba samahani wale wote walioniandikia wakiuliza juu ya kuchelewa kuweka makala za Padri Karugendo na zile za Freddy Macha nilizowaahidi. Nina makala zao nyingi na zenye ujumbe mzito kwetu sote. Nitapandisha moja moja kadri muda unavyoruhusu. Pia nitajibu barua pepe zenu zote, ingawa nitachelewa. Ombi la kuweka baraza la majadiliano nimelipokea. Ngoja nitumie lugha ya "wana si-hasa": ombi lenu linashughulikiwa.
Mada ninayoandaa imenikamata hasa. Nina rundo la machapisho ya kusoma, vitabu, tovuti za kutembelea, na wanablogu wa kuwasiliana nao. Mniwie radhi nikitokomea. Tuko pamoja. Tuendelee kunoa akili zetu na kusafisha ukurutu wa kasumba, utegemezi, na kutokujiamini. Wakati ni huu.
Kuna barua kadhaa za wasomaji na marafiki zangu ambazo nimezipenda mno. Nazo nitazipandisha hapa mzisome. Zitakuwa chakula murua kwa ajili ya fikra zetu.

NIMEJICHIMBIA

Nimekuwa kimya kidogo. Sababu ya ukimya huu ni kuwa nimejichimbia kwa maandalizi ya mada nitakayoitoa mwezi ujao katika mkutano wa masuala ya teknolojia na watu weusi utakaofanyika katika chuo kikuu cha California, Santa Barbara. Mkutano huo unaitwa Afrogeeks: Global Blackness and the Digital Public Sphere. Mada yangu inahusu blogu zinazotumia lugha za Kiafrika. Kwa wale waliomsoma Ngugi katika "Moving the Centre" na "Decolonising the African Literature," ninajaribu kupanua hoja kuu katika vitabu hivi (na vingine kama hivi). Ninatazama changamoto mpya kwa tamaduni na lugha za Kiafrika katika zama hizi za maarifa/habari, na utandawazi. Habari zaidi za mkutano huo nenda hapa. Mkutano kama huu ulifanyika pia mwaka jana. Tazama hapa.

4/04/2005

URITHI WA TIMBUKTU

Unayafahamu maandiko ya Timbuktu? Hapa.

UMEISIKIA SIMPYUTA?

Moja ya tatizo kubwa linalokumba nchi masikini duniani (kutokana na wizi wa viongozi wao na mfumo mbaya wa biashara duniani na uzembe wa wananchi wa nchi hizo wanaochagua watawala wezi) zinazotaka wananchi wake kushiriki kikamilifu katika zama hizi za habari/maarifa ni upatikanaji wa zana za mawasiliano kwa bei nafuu. Wafuatiliaji wa suala hili wanadai kuwa aina mpya ya kompyuta iitwayo Simpyuta (Simputer) inaweza kuwa ni moja ya majawabu mengi ya tatizo hili. Soma hapa na hapa kuhusu simpyuta.

MTANDAO USIWAYA KWA CHUPA YA MAJI HUKO MALI!

Kuna miradi ya kibunifu sana inakuja ili kurahisisha usambazaji wa zana mpya za mawasiliano na habari. Nchini Mali kuna mradi wa kujenga mitandao usiwaya (wireless networks) kwa kutumia chupa za maji! Tazama hapa mwenyewe.

4/03/2005

BLOGU MPYA ZA KISWAHILI

Hayawi, hayawi...
Zimekuja blogu nyingine mbili za Kiswahili zinazoandikwa na waandishi wa habari toka kule kunakodaiwa kuwa ndio mji mkuu wa Tanzania (huku wakuu wenyewe wakijishindilia Dasalama). Blogu hizo ni ile ya Ramadhani Msangi inatosema: Mama Yangu, Wamekunywa Hata Uji wa Mgonjwa. Kongoli hapa. Nyingine ni ile ya mwandishi Hudson Kazonta inayosema: Wamekula Mbuzi...Wakaota Mapembe. Kongoli hapa. Iko blogu nyingine ninayoisubiri kwa muda mrefu sana inayokuja toka Australia. Kaa chonjo!

WEBOPIDIA: KAMUSI YA MISAMIATI YA TEKNOLOJIA YA TARAKILISHI

Kama unasumbuliwa na misamiati mikubwa mikubwa inayohusu teknolojia ya tarakilishi, nenda kwenye kamusi ya teknolojia iitwayo webopidia. Hapa.

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com