5/31/2005

Creative Commons ndani ya Yahoo!

Kwanza kabisa nenda hapa kwa undani kuhusu mradi wa Creative Commons. Kisha jua kuwa unaweza kutafuta kazi zinazotolewa kwa modeli ya Creative Commons ndani ya Yahoo! Hapa.
Creative Commons, tofauti na sheria za kibepari zilizopo za hatimiliki, inawapa uwezo zaidi wananchi, watunzi, wasanii, waandishi, wanamuziki, n.k., kuamua kazi zao zitumike vipi na umma. Sheria za hatimiliki zilizopo zimejengwa juu ya mantiki ya kibepari na kibinafsi ya "Haki zote zimehifadhiwa." Lakini Creative Commons inakuja na mantiki ya kijamaa na kibuntu isemayo "Baadhi ya haki zimehifadhiwa," au "Hakuna haki zilizohifadhiwa."
Huu ndio ulikuwa msingi wa mkutano wa Commons-sense. Na haya ndio mapinduzi yanayokuja kutokana na teknolojia mpya za habari na mawasiliano.

5/30/2005

UNAWEZA KUTAZAMA VIDEO KWA MIAKA 68?

Paula LeDieu, aliyewahi kuwa mkurugenzi wa idara ya nyaraka huru za shirika la habari la BBC, aliongea jioni ya tarehe 26 katika mkutano wa Commons-Sense. Alitumia kama dakika ishirini hivi kuzungumzia uamuzi wa shirika hilo kutumia modeli ya hatimiliki ya Creative Commons. Mradi uitwao The Creative Archive unaruhusu wakazi wa Uingereza (kwakuwa kodi yao ndio inaendesha shirika hili) kutumia kwa njia zozote zile (isipokuwa kibiashara) nyaraka zote za shirika hilo. Mradi huu ulianza rasmi mwaka jana.

Kwakuwa BBC ilianzishwa mwaka 1922, rundo la nyaraka ambazo imehifadhi ni kubwa kiasi ambacho inakupasa ukae mbele ya luninga yako ukitazama bila kuzima kwa miaka 68, masaa 24 kwa siku! Utaweza?

TAZAMA VIDEO YA MAHOJIANO YANGU AFRIKA KUSINI

Nimewasili Babiloni. Safari nzima nilikuwa najiuliza, "Hivi nitablogu nini na nini nitaacha?" Kwanza hata pa kuanzia sijiu. Nimeamua kuwa nitakuwa nablogu kila siku mambo kadhaa yaliyotokana na mkutano wa Commons-sense; mambo niliyojifunza, watu niliokutana nao, miradi mbalimbali inayotumia zana mpya za mawasiliano Afrika, niliyoona katika jiji la Egoli/Jozi (majina ya jiji la Johannersburg), mapana na marefu ya dhana hii ya "creative commons" (bado natafuta tafsiri yake sahihi ya Kiswahili), n.k.

Ndio nimeamka nataka kunywa chai. Ningependa kwa sasa utazame video hii ya mahojiano niliyofanya na New Media Lab ya chuo kikuu cha Rhodes. Bonyeza hapa uitazame.

5/28/2005

Naondoka leo

Mshikaji wangu, Donald (jamaa nikitaka kumwelezea sijui nitaanzia wapi), ananizungusha katika jiji la Egoli. Tumetoka katika mahakama ya katiba ambayo ilikuwa ni gereza liitwalo Old Fort. Nimepita kwenye mgahawa huu kutazama jambo fulani kwenye mtandao. Picha na yote yanayohusu mkutano wa Commons-Sense ni mpaka nitakapowasilia Babiloni kwa Joji Kichaka mwizi wa kura. Ninaondoka leo usiku.
Uhuru!

5/27/2005

MAHOJIANO KUHUSU BLOGU ZA KENYA REDIO YA OPENS SOURCE

Nimefungua barua pepe toka mviringo wa blogu za Kenya (Kenya Unlimited) kuhusu mahojiano wiki ijayo kuhusu blogu za Kenya kupitia redio ya Open Source. Fuatilia.

Mkutano wa Commons- Sense unaendelea. Asubuhi nilichelewa baada ya kulala saa kumi alfajiri. Basi liliniacha ikabidi niende kwa mshikaji mmoja Mkenya akanileta. Ingawa tulipotea njia niliwahi mduara uliokuwa ukijadili blogu (blogging the commons). Mduara huu nadhani ndio bora katika majadiliano yote toka mkutano uanze. Kama nilivyoahidi nitawapa kwa undani yaliyosemwa na yanayofanyika huku Afrika kuhusiana na blogu na zana nyingine za mawasiliano.

5/26/2005

BLOGU MOJA KWA MOJA TOKA MKUTANO WA COMMONS-SENSE

Wanafunzi 15 na walimu wawili wa maabara ya uandishi wa zana mpya za habari katika idara ya uandishi wa habari ya chuo kikuu cha Rhodes hapa Afrika Kusini wanablogu moja kwa moja toka mkutanoni. Nenda hapa ufuatilie kila kinachotendeka kila dakika!

5/25/2005

MKUTANO WA COMMONS-SENSE

Nimewasili hapa jana baada ya safari ya masaa 17 hivi. Nadhani nilitakiwa kuoga na magadi kabla ya kuondoka ili kuondoa kisirani kwani begi langu la nguo halikufika! Litafika leo usiku na nitalipokea kesho! Niende nikanunue nguo mpya? Nisubiri
Kwa wale wasiofahamu, ninahudhuria mkutano unaoitwa Commons-Sense ulioandaliwa na chuo kikuu cha Wits, Creative Commons (Afrika Kusini), na Links. Mkutano huo unafanyika hapa katika jiji la Egoli ( jina la Kizulu la jiji la Johannersburg). Shughuli rasmi zitaanza leo jioni kwa tafrija ya mkia wa jogoo (kwa kiingereza wanaita "cock tail"). Tayari nimekutana na watu wawili ambao nao wanahudhuria mkutano huu. Dada mmoja toka Kenya na mwingine toka Marekani.
Nenda hapa kwa taarifa zaidi juu ya mkutano huu.
Jana usiku, ingawa nilikuwa nimechoka, sikujisikia kulala. Nilishuka chini (ninakaa hapa) kwenda kuongea na waswahili wenzangu ambao kazi zao ni ulinzi, ufagizi, kufungua milango, n,k. Tsedu ni mlinzi wa usiku hotelini hapa. Anaishi kitongoji cha Alexandra. Tsedu ni rasta: anamuenzi Mfalme wa Wafalme, Simba wa kabila la Yuda Haile Selassie I, Jah! Rastafari!
Tsedu alinivunja mbavu. Baada ya kuniambia kuwa yeye ni rasta na anapenda sana kusikiliza muziki wa hisia na mafunzo, Rege, nilimuuliza kama anampenda Lucky Dube. Akanitazama kwa mshangao na kusema, "Dube hapigi rege. Ile sio rege!" Tsedu anawasikiliza wanamuziki kama Culture, Burning Spear, Bob Marley, Mutabaruka (yule mshairi anayetembea pekupeku), Luciano, n.k. "Rege ni mafunzo, ni tenzi za rohoni, ni mashairi ya kiroho..." Tsedu ananiambia.
Karibu kila wimbo niliomtajia wa wanamuziki anaowasikiliza, alikuwa amekariri maneno yake na hata ufafanuzi wa jinsi ujumbe wa nyimbo hizo unavyoendana na hali ya kisiasa, kiuchumi, na kiutamaduni duniani hivi sasa. Nilipomtajia wimbo wa Burning Spear uitwao "Days of slavery." Alitabasamu huku akitikisa kichwa. Kisha akaanza kuuimba. "Watu wengi wanaposikiliza huu wimbo wanafikiria mambo yaliyotokea miaka mingi iliyopita. Hapa Afrika Kusini utumwa anaozungumzia Burning Spear upo hadi leo."
Tulipiga gumzo na Tsedu kwa masaa kadhaa...nadhani nilienda kulala saa tisa. Nilipomtaja Steve Bantu Biko, Tsedu alitazama chini, uso wake ukajaa huzuni. Alikaa kimya kwa muda kisha akasema, "Black consciousness." Black Consciousness ni jina la falsafa na itikadi aliyokuwa akihubiri mwanamapinduzi Biko. Baada ya muda kidogo alinieleza kwa kina jinsi Biko alivyouawa kinyama. Alivyoburuzwa akiwa amening'inizwa nyuma ya gari katika barabara ya kokoto. Uchi wa myama. Alipomaliza kunieleza kwa undani na hisia kali niligundua kuwa sikuwa ninafahamu kwa kina yaliyotokea siku za mwisho wa uhai wake. Maelezo yake yalinitia hasira na huzuni kwa wakati mmoja. Hadi sasa bado kuna donge limekwama kooni.
Nilipomuuliza Tsedu juu ya kitongoji anachoishi, visa alinieleza visa ambavyo vimenijaza huzuni kubwa. Anasema kuwa maisha wanayoishi Waafrika katika vitongoji mbalimbali nchini humu hayana thamani yoyote. Vifo kutokana na ukimwi, ujambazi wa kutumia silaha vimekuwa ni kitu cha kawaida. "Nikiwa nyumbani nikasikia mlio wa risasi huwa ninaendelea na shughuli zangu. Hata watoto wangu wamezoea. Kila mtu kazoea. Hakuna anayeshtuka. Tumekuwa sugu. Tumekuwa viziwi. Tumekuwa vipofu. Hii ndio njia pekee ya kuendelea kuwa na akili timamu. Bila hivyo utarukwa na akili au utakata tamaa na kujiua. Anasema majambazi katika vitongoji vya weusi wamefika hatua ambayo hakuna kinachowazuia kupora mtu yeyote na saa yeyote. "Majambazi wanampora mtu pembeni yako, unatazama na kuendelea na shughuli zako." Ananiambia.
Anasema kuwa siku moja aliporwa simu ya mkono. Kawaida akiwa vitongojini hapendi kutumia simu yake. Siku hiyo alisahau kuizima. Akiwa anapita mtaani, simu ikalia. Jamaa watatu wakamfuata, mmoja wao akamwambia, "Pokea hiyo simu. Ukishamaliza kuongea tupe simu yetu." Wakati wanamwambia hivyo mmoja wao alikuwa amechomoa bastola.
Nitakutana na Tsedu leo usiku baada ya ufunguzi rasmi wa mkutano na tafrija ya mkia wa jogoo. Usisahau kutembelea tovuti ya mkutano huu. Nitakuwa ninawapa taarifa mbalimbali kadri mkutano unavyoendelea. Ninakwenda kutembea mjini hadi jioni. Sijui nikanunue bastola...maana nataka kwenda ile mitaa ninayoambiwa kuwa nisithubutu kupeleka unyayo. Huko ndio ninataka kwenda. Niombeeni!!!!
Sobonana futhi (tutaonana baadaye kwa Kizulu).

5/22/2005

MVIRINGO WA BLOGU ZA KISWAHILI

Nilikosea kiungo cha mviringo wa blogu za Kiswahili. Mviringo huu hapa.

5/17/2005

BLOGU ZA LUGHA ZA MAKABILA YA AFRIKA

Kwanza nilitangaza blogu ya Kishona. Hapa. Kisha nikatangaza blogu ya Kichagga. Hapa. Sasa rafiki yangu, Mokhtar, toka Morocco ameanza kublogu kwa lugha ya Kiberber, Tamazeight. Mokthar ni anafundisha Kiarabu katika chuo hiki. Blogu yake hapa. Nina mambo mengi ya kuandika na kutundika lakini muda umekuwa mdogo. Jumamosi ndio siku ninaongea katika mkutano wa Afrogeeks kuhusu blogu za Kiswahili na jumatatu ninaondoka kwenda Afrika Kusini kwenye mkutano wa Commons-Sense.

5/16/2005

AMINI USIAMINI...BLOGU YA KICHAGGA IMEKUJA

Baada ya kuanza kufumuka blogu za Kiswahili, mwanadada toka kule kwa Mangi Horombo, chini ya mlima wa Ruwa (Kilimanjaro), amekuja na blogu kwa lugha ya Kichagga. Mtembelee Mtafiti na blogu yake hapa. Mtafiti hivi sasa yuko masomoni nchini Marekani ila anaendelea kuenzi utamaduni wake.

MVIRINGO WA BLOGU ZA KISWAHILI

Shukrani za dhati zinamwendea ndugu yetu Maitha. Ametupatia mviringo wa blogu za Kiswahili. Tembelkea mviringo huo hapa.

5/13/2005

NINAFANYA MAHOJIANO NA REDIO YA OPEN SOURCE

Dakika hii ninavyoandika ninasubiri dakika chache kabla ya kufanya mahojiano kuhusu blogu na redio ya Open Source. Nenda hapa.

5/10/2005

MKUMBOKRASIA!

Idya wa blogu ya Pambazuko kanipa msamiati mpya: Mkumbokrasia. Mkumbokrasia ndicho kimekuwa chakula, maji, na chai ya Watanzania hasa baada ya kuchaguliwa Jakaya Kikwete. Nimekaa kimya, nimesoma yanayotokea Tanzania, nimechambua hoja za wananchi, vijana kwa wazee. Nimeulizwa niseme ninamwonaje Kikwete. Sasa Idya kanipa msukumo wa kukaa chini na kuandika mawazo na mtazamo wangu. Nitatumia msamiati huu wa "mkumbokrasia" kujenga hoja zangu za msingi. Kaa tayari kumeza au kutema vidonge...hiyo itakuwa ni shauri yako. Soma makala mpya za Padri Karugendo na blogu nyingine za Kiswahili wakati ninaandaa jibu kuhusu ninamwonaje Kikwete.

KARUGENDO: TUACHENI TUTETEE MATUMIZI YA KONDOMU

Haya. Kuna makala nne kabambe za Padri Karugendo. Zinaitwa: Tuacheni Tutetee Matumizi ya Kondomu, Tumwogope Mungu kwa Matendo Yetu Yote Kila Siku na Kila Wakati, Papa Benedikto ni Rafiki wa Tanzania, na Elimu, Vijana, na Uchumi. Bonyeza juu ya makala unayotaka kuisoma. Kumbuka makala zake za nyuma ziko katika kona yake, Kalamu ya Padri Karugendo chini ya makala zangu naFreddy Macha.

5/08/2005

DA MIJA: MWANABLOGU MPYA WA KISWAHILI KAINGIA

Tunampokea kwa shangwe, nderemo, vifijo, nyimbo, vigelegele, na ngoma za ukae mwanablogu mwingine mpya wa Kiswahili. Huyu ni dada yetu Da Mija anayeblogu toka Amsterdam, Uholanzi. Sasa tuna dada zetu wanne wanaoblogu kwa Kiswahili. Tuwakaribishe na kuwatia moyo. Kila blogu ya Kiswahili inapojitokeza ninapata furaha isiyoelezeka. Kongoli hapa umsome.

NIPE AYA!!!!: MAKALA MBILI MPYA

Nipe Aya! ni moja ya makala mbili mpya ambazo nimepandisha hapa ndani. Kaba ya kusoma makala hizi ni vyema ukasoma kwanza makala ya Wazee Afrika ni Vyuo Vikuu ambayo iko katika kona ya makala zangu, chini ya picha yangu. Makala ya kwanza leo inaitwa: Soma Anga, Mawingu, na Nyota Kama Kitabu. Bonyeza hapa. Ya pili ndio hii ya Nipe Aya! Bonyeza hapa.

WALE WAZUNGUMZAJI WA KISWAHILI...

Kama wewe ni mzungumzaji wa Kiswahili, unaipeda lugha hii na una muda, tafadhali shiriki katika kujenga kamusi elezo ya kiswahili iliyoko katika mfumo wa wiki. Teknolojia ya wiki inawezesha mtu yeyote kushiriki katika kuhariri na kuandika kamusi hii. Ninatafsiri orodha ya mambo ya msingi yanayopswa kuwemo katika kamusi hii. Nenda hapa. Ukiwa na swali lolote kuhusu hili unaweza kuniandikia. Lakini kwa ujumla teknolojia ya wiki ni rahisi sana kwa mtu yeyote yule kuitumia.

5/07/2005

MKUTANO AFRIKA KUSINI / SKOLASHIPU

Niliutaja huu mkutano siku za nyuma. Usiache kuufuatilia. Ni ule mkutano wa Commons-Sense huko Afrika Kusini. Nenda hapa. Pia kama ni mwanablogu au mtafiti wa masuala ya zana mpya za mawasiliano na habari unaweza kupewa skolashipu. Fanya hima. Nenda hapa kuna fomu fulani ya kujaza.

5/05/2005

BLOGU NYINGINE TENA JAMANI YA KISWAHILI!

Tanga kunani? Kuna wimbo ule wanasema kuwa Tanga watu huoga na maji yenye viungo kama mdalasini na iliki! Na Dokta Remmy, katika kibao cha Mariamu anasema, "Waja leo, warudi leo, Tanga mbali..." Sasa kaingia binti kutoka Tanga katika ulimwengu wa blogu za Kiswahili. Blogu yake inaitwa Wanawake na Maendeleo. Nenda hapa umsome na kumkaribisha.

MAONI NA FALSAFA ZA SHUJAA MARCUS GARVEY

Kuna wakati unasoma jambo, linakuingia hasa hadi unaamua kuacha kusoma na kwenda kunywa maji, kujisaidia, kujinyoosha, kutengeneza chai, kisha unarudi tena kusoma. Ndio imenitokea leo nilipotembelea blogu ya Mwandani. Nimekwenda hapo nikakuta amemnukuu shujaa Marcus Mosiah Garvey. Nimechukua nukuu hiyo. Hii hapa:

Ni wachache tu kati yetu, ambao wanaelewa ni kitu gani kinachomfanya mtu awe mtu!Namaanisha -Mtu asiyeweza kufa moyo; mtu asiyeweza kukata tamaa;
Mtu asiyetegemea wengine wamfanyie yale anayoweza kuyafanya yeye mwenyewe;
Mtu asiyemlaumu Mungu, asiyelaumu mazingira;
mtu asiyelaumu ‘bahati mbaya’ kwa hali yake kimaisha;
Bali yule mtu awezaye kutoka na kujitengenezea mazingira yanayomwezesha kuishi.
Kweli nawaambia, ikiwa sisi watu weusi milioni mia nne tungekuwa tunajitambua,
Na tungetambua kwamba ndani yetu tunao uwezo na haki,
Na kwamba tunayo mamlaka kamili,
Ama kwa hakika nawaambieni, mnamo masaa ishirini na nne tu yajayo tungekuwa na taifa jipya,
Tungekuwa na dola iliyosimama kisawasawa,
Si kutokana na matakwa ya watu wengine wowote ya kutaka kutuona tunatengenekewa,
Bali kutokana na moyo wetu dhabiti wa kutakaka kujiinua,bila kujali watu wengine humu duniani wanatufikiriaje.
-Marcus Mosiah Garvey

BLOGU MPYA YA KISWAHILI YA MTAWA MWEUSI

Bakanja ni mtawa mweusi. Ameanza kublogu kwa kiswahili. Mwili unanisisimka kwa jinsi ambavyo blogu za Kiswahili zizidi kuchomoza. Wanablogu wengine nimeona blogu zao ila hawako tayari kujitangaza, bado wanazifanyia kazi chini kwa chini. Mtembelee Bakanja hapa.

WAKATOLIKI NA MATAMBIKO, BLAIR NA AFRIKA!

Rafiki yangu kanitumia ujumbe alioandikiwa na rafiki yake. Ujumbe mfupi ila kataja mambo mengi. Siwataji majina yao ila nauweka ujumbe wenyewe hapa. Huo hapo chini:
Kwanza nimesikitishwa sana na mambo ya matambiko na uchawi uliokuwa unafanyika kwenye uchaguzi wa Papa. Hivi ule moshi mweusi na mweupe ni nini kama sio uchawi au tambiko. Hivi mwafrika ndio akifanya mbwembwe na matambiko kama vile ndio unakuwa uchawi ila mzungu yeye akifanya ni "utaratibu tu uliozoeleka kwa muda mrefu." Hivi na hii Tume ya Blair inayotaka kumaliza matatizo ya nchi za Afrika umeiona? Ina watu wanaitwa maprofesa mle ndani. Mimi nadhani wale ni maprofesa wa ujinga maana akili zao ni ndogo kuliko binadamu yeyote niliyewahi kumuona. Hawajawahi kusoma historia na hoja zao ni hafifu sana. Eti wao hawajui matatizo yao na wala hawajui namna ya kuyatatua mpaka wasaidiwe na Blair. Kuhusu uchaguzi wa Tanzania mimi sitaki kabisa kusumbua kichwa changu kuhusu nani atakuwa Rais. Huwa ni rahisi sana kumtambua mwenye uwezo kati ya wanyonge ila ni ngumu sana kumtambua mpuuzi sana kati ya wapuuzi wengi. Hivi ni nani angehisi kuwa mwaka 1995 nchi hii ingemhitaji mtu mwenye sera za kipuuzi kama hizi za Mkapa na utandawazi wake? Hivi mtu kama hauwezi kutumia rasilimali zako dawa ni kuzitoa kwa mtu mwingine ili azitumie badala ya wewe kujenga uwezo wa kuzitumia hata kama ni miaka 500? Nadhani ukibahatika kujua ni nani mpuuzi kuliko wagombea hao wote utamjua Rais anayefuata maana nadhani hizi nchi za kiafrika ili sifa zao zitimie ni kuwa na kiongozi mpuuzi.

5/03/2005

PAPA BENEDIKTI: PIGO KWA TEOLOJIA YA UKOMBOZI

Padri Karugendo kaja na makala mbili. Ya kwanza inasema Papa Benedikti: Pigo kwa Teolojia ya Ukombozi. Bonyeza hapa uisome. Nyingine inasema: Mungu Hajakataza Wanawake kuwa Mapadri au Wachungaji. Isome hapa. Makala zake nyingine ziko kwenye kona ya makala zake iitwayo Kalamu ya Karugendo. Iko chini ya makala zangu na za Freddy Macha, upande wa kuume wa blogu hii.

BLOGU NYINGINE YA NGUVU LA KISWAHILI HIYOOO....

Mwanablogu huyu nilikuwa nikimsubiri kwa hamu sana. Fikra zake ninazifahamu kwa muda mrefu sana...toka mwaka 1992? 1993? Ninafahamu amesimama wapi. Ameanza kublogu rasmi kwa Kiswahili. Blogu za kiswahili, kama ninavyosema kila ninapotangaza blogu mpya, zinakuja kwa mwendo wa maringo. Hakuna haraka. Blogu hii mpya inaiwa Pambazuko. Anakuja na ujumbe huu: Wakati wa Kubadili Fikra ni Huu. Anaongeza: Badili Fikra, Badili Mawazo, Badili Mtazamo. Bonyeza hapa umtembelee.

MGOMBEA "URAHISI" WA CCM

Kamati kuu imewapitisha Kikwete,Mwandosya, Sumaye, Salim na Kigoda kuwa katika orodha ya watano ambao watachujwa ili kupata watatu bora kwa "urahisi" wa muungano. Soma hapa.

BLOGU NYINGINE YA KISWAHILI YA BINTI WA KITANZANIA

Wahenga walituambia kuwa mwenda pole hajikwai. Ndivyo wafanyavyo wanablogu wa kike wa kiswahili. Wanakuj polepole. Kwanza alijitokeza Zainab. Sasa kajitokeza dadetu Martha na blogu yake nzuri iitwayo "Kutoka Ugogoni." Msome hapa. Karibu Martha Mtangoo.

Ugogoni kwa wale wasiofahamu ni Dodoma, katikati ya Tanzania. Kabila kubwa mkoani hapo ni la Wagogo. Dodoma, kwa mujibu wa sirikali, ndio mji mkuu wa Tanzania. Usinihoji zaidi kuhusu hili. Sidhani hata kama viongozi wenyewe wanaweza kukwambia kwanini Dodoma ndio mji mkuu na sio Dar es Salaam.

5/02/2005

CHE GUEVARA ALIKUWA NA JINA LA KISWAHILI

Kumbe Che Guevara na Wakuba waliokuwa msituni kule Congo wakipambana na mabeberu walijifunza Kiswahili maana ilikuwa ndio lugha ya mapambano. Pia walijipa majina ya Kiswahili. Shujaa Che Guevara jina lake la Kiswahili lilikuwa ni Tatu. Nimeipata katika insha ya Mulokozi niliyoigusia muda mfupi uliopita. Unaweza kuisoma mwenyewe hapa. Halafu kama una nafasi/uwezo wa kuiona au kununua filamu kuhusu Che ya The Motorcycle Diaries fanya hivyo. Hutajilaumu. Kuhusu filamu hiyo bonyeza hapa. Na ukitaka kusoma au kusikiliza hotuba zake nenda hapa.

KISWAHILI: LUGHA YA KITAIFA NA KIMATAIFA

Nimemaliza kusoma insha nzuri sana iliyoandikwa na M. Mulokozi wa Taasisi ya Utafiti wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam. Bonyeza hapa nawe ufaidi.

UMEISIKIA "Initiative B@bel"?

Wakati ambapo kuna lugha zaidi ya 6000 duniani, zaidi ya asilimia 90 ya mambo yote yaliyoko kwenye mtandao wa kompyuta yako kwa lugha 12 tu! Soma hapa kuhusu mradi wa Initiative B@bel. Je kwa mwendo huu tunaweza kusema kuwa dunia imeingia kwenye zama za jamii-maarifa/ jamii-habari?

MKUTANO WA UNESCO WA LUGHA NA TAMADUNI MBALIMBALI

Mwezi huu huko Mali kuna mkutano kuhusu umuhimu wa kushamiri kwa lugha na tamaduni mbalimbali kwenye mtandao wa kompyuta. Soma hapa. Ajenda ya mkutano huo hii hapa.

KUMBE KUNA PAPA WAWILI DUNIANI!!

Kuna bwana nadhani amechanjiwa kejeli. Majuzi kauza anuani ya barua pepe ya Papa Benedikto katika mnada wa mtandaoni wa eBay. Soma habari hiyo hapa na hapa. Hakuishia hapo, kajitanga kuwa yeye ni Papa wa mtandaoni na kuanzisha dini ya kukanganyikiwa! Blogu yake hii hapa.

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com