6/24/2005

Marekani, Marekani, Marekani...

Sirikali ya Marekani inayoongozwa na mwizi wa kura, Joji Kichaka, inanichefua kupita kiasi. Wakati wakianza kushawishi dunia bila mafanikio kuhusu uvamizi dhidi ya Iraki, moja ya sababu kuu walizotoa ni kuwa nchi hiyo imekuwa ikizuia wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kukagua maeneo yanayoaminika kuwa yalikuwa yanatengeneza silaha za sumu. Watawala wa nchi hii wakauliza, "Kama Iraki haitengenezi silaha kwanini inakataza wakaguzi wa Umoja wa Mataifa? Kuna nini kinafichwa?"
Sasa kichekesho cha siasa za beberu huyu ni hiki: toka mwaka 2002 (leo ni 2005) Umoja wa Mataifa umekuwa ukiomba ruhusa toka sirikali ya Marekani ili wakaguzi wake waende wakatembelee wafungwa walioko ghuba ya Guatanamo. Hadi dakika hii Marekani haijakubali kuruhusu wakaguzi hao. Ni kitu gani kinafichwa?
Taarifa za mateso na unyama uliokithiri unaofanywa na Marekani dhidi ya wafungwa zinatisha. Majuzi tulisikia kuwa badala ya kutumia karatasi maalum za chooni, askari wa Marekani hapo Guantanamo walitumia Kurani. Hivi Marekani imeishiwa kiasi cha kushindwa kununua karatasi za chooni?
Kwanini wakaguzi wa Umoja wa Mataifa hawaruhusiwi? Ukweli ni kuwa wakaguzi hao wakiruhusiwa kuonana na wafungwa, habari za kuteswa kwao tukazisikia, dunia nzima itatambua kuwa sirikali ya Marekani haina tofauti yoyote na sirikali ya Taliban au ya huyo Saddam Hussein waliyemgeuka. Ukitaka kujua ukweli wa serikali hii tazama marafiki zake wakubwa: Saudi Arabia, Israeli, Equatorial Guinea, Pakistani, n.k. Usisahau pia kuwa sirikali za Taliban na Saddam Hussein zilikuwa ni maswahiba wa kufa na kuzikana na Marekani kwa miaka mingi. Ukitaka kumfahamu mtu kwa undani, tazama marafiki zake. Ndivyo hivyo hata kwa sirikali.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com