7/08/2005

Mchezo umekwishi kule Gleneagles

Ni saa tisa usiku. Nilikaa Gleneagles hadi saa sita usiku. Nilikuwa kati ya watu wa mwisho kuondoka maana nilijua nikija nyumbani nikiona kitanda nitalala, kama ambavyo nitafanya nikishamaliza kuandika hapa. Wakati naondoka kuelekea kwenye basi nilitazama kila upande bila kuamini kuwa sehemu iliyokuwa imejaa askari na watu wenye kamera, beji zinazoning'inia shingoni (kila mtu ilikuwa lazima awe na beji), makaratasi, kalamu, kompyuta za mapajani, wahudumu, n.k. ghafla imekuwa mahame. Askari walikuwa wameyeyuka. Wanaharakati wametoweka. Waandishi wamebaki wachache, nao ndio wanaondoka. Helikopta hazipo tena angani.
Natembea polepole na begi langu nikijiuliza, "hivi nilikuja kufanya nini hapa?"
Nilijiona kama mtu anayetoka ndani ya chumba cha maigizo akirudi kwenye dunia halisi. Kuna mwanafalsafa mmoja, sikumbuki ni nani, alisema kuwa dunia hivi sasa imekuwa kitu alichokiita, "media spectacle." Yaani maisha ni kama vile kioja kwa ajili ya vyombo vya uongo (vyombo vya habari). Na hivyo ndivyo ilivyokuwa pale Gleneagles. Mchezo wa kuigiza unaofanyika kila mwaka kwa jina la G8 Summit. Mchezo huu utaendelea mwaka ujao kule Urusi.
Nimepitia vyombo kadhaa vya habari kuona maoni ya watu juu ya tamko la makuhani wakuu wa ubepari la kuongeza "msaada" kwa nchi za Afrika. Wako wanaounga mkono na wanaopinga. Watu kama akina Bono na Geldof wakiunga mkono nitawaelewa maana wanataka kutudanganya kuwa kampeni zao kama Live 8 ndio zimefanya wezi hawa wa maliasili za Afrika (wakishirikiana na Waafrika) wakaamua "kuisaidia" Afrika. Akina Bono wanataka kutuambia kuwa akina Kichaka wameguswa na kauli ya walimwengu! Hivi unadhani watu bilioni mbili wakisema jambo, na mabosi watatu wa kampuni la kipebari kama Halliburton wakisema jambo, Joji Kichaka atasikiliza kina nani? Watu bilioni mbili? Thubutu!
Nikiwa ndani ya basi kabla ya kusinzia nilijichekea mwenyewe: baada ya tamko la "kuisaidia" Afrika kwa dola bilioni 50 (sijui nyumba ngapi zitajengwa ufukweni mwa bahari, na akaunti ngapi zitafunguliwa ughaibuni, na suti ngapi na vito vya thamani vitanunuliwa na watawala wa Afrika kwa hela hii) kila mwandishi wa kizungu alikuwa akiona mtu mweusi anataka kumhoji. Nilitamani ningevaa bango kusema, "Sitaki kuhojiwa!" Niliona kuwa hata wakati wa mazungumzo na waandishi wa habari ya Blair, waandishi weusi walipewa nafasi ya juu kidogo tofauti na ilivyo kawaida katika mikutano mikubwa kama hii. Ghfala ngozi nyeusi ilionekana kama vile sijui ni kitu gani. Nyani wamejua kuvaa nguo?
Nililala sehemu kubwa ya safari ya dakika tisini toka Gleneagles hadi Edinburgh. Kisha teksi hadi Royal Circus namba moja. Ndipo nipo sasa na ninakaribia kwenda kulala.
Kesho asubuhi tunarudi London, jiji nilichukialo kwa mbio zake za kuwahi basi, treni, msongomano wa watu, na habari hizi za ugaidi zimenifanya nisiwe na raha ya kurudi pale.

Pazia limefungwa. Mchezo umeisha. Washeni taa. Twendeni nyumbani.

1 Maoni Yako:

At 7/09/2005 05:49:00 AM, Blogger Maka Patrick Mwasomola said...

Kweli pazia limefungwa inabidi tuwashe taa na kwenda nyumbani.Na ni kweli kabisa kati ya watu bilioni mbili na wale "mafogo" watatu kwa asilimia mia moja watakaosikilizwa ni wale watatu.
Ni sawa pia nyumba zitajengwa ufukweni,suti zitanunuliwa na zurich zitahifadhiwa hazina nyingi tu kwa kiasi hicho cha pesa.
WAO NI MTI MKUBWA SANA SISI NI SHOKA DOGO LAKINI LISILO NA MAKALI NA AMBALO WALA HALIKO TAYARI KUUKATA MTI HUO NA KUUANGUSHA CHINI!

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com