9/02/2005

Rangi wa "wanaoiba" na rangi ya "wanaochukua"



Baadhi wameshinda kufungua picha nilizokuwa nazungumzia zinazoonyesha chembechembe za mtazamo wa kibaguzi ambao umejificha kwenye vyombo vya habari hapa Marekani. Bonyeza juu ya picha kuikuza ili usome maelezo yake vizuri. Tazama maelezo ya picha ya mweusi yanaonyesha kuwa yeye ni kibaka. Na picha za weupe, maelezo yanaonyesha kuwa wao wamejichukulia tu chakula (ingawa hawakupewa na wenye duka)!

Hivi sasa taarifa zaidi zinaanza kutoka katika vyombo vya habari kuonyesha jinsi ambavyo rangi ya wahusika wengi katika janga la Katrina imechangia kufanya juhudi za msaada kwenda polepole zaidi ya kinyonga. Wakati huo huo vyombo vya habari vimechukua habari ya maduka kuvunjwa kuwa ni kubwa zaidi ya maelfu ya watu wasio na chakula, madawa, maji, makazi, n.k. Wakati ambapo barabara zimejaa maiti zinazoliwa na mapanya. Wakati ambapo watoto wachanga wanakufa kwa njaa...ndani ya Marekani! Hata serikali yenyewe imetuma wanajeshi, sio kwenda kuokoa watu bali kulinda usalama wa maduka na mali nyingine za matajiri. Askari hao wameambiwa wasisite kufyatua risasi, sio kuvunja mguu bali kuua. Baadhi ya watu ndio wanang'amua kumbe ni kweli kwenye ubepari kitu muhimu ni kile kiitwacho "private property" zaidi ya uhai na heshima ya binadamu masikini. Ndio maana unaona askari wanatumwa kwenda kuzuia uporaji wa mali za matajiri na sio kusaidia masikini wasiojua waende wapi au wafanye nini. Wamepoteza hata kile kidogo walichonacho.

1 Maoni Yako:

At 9/03/2005 06:14:00 PM, Blogger Jeff Msangi said...

Ndesanjo,
Ahsante kwa taarifa hii ya chembe za wazi za kibaguzi.Ningefurahi kama ungenisaidia masuala haya; Wamarekani weusi hivi sasa wanasemaje haswa?Wanapanga kufanya nini?Kwanini siku zote wamedhani kwamba majanga kama hayo hayawahusu wao kama binadamu wengine?Nini chanzo cha umbumbumbu huu?Kwanini Wamarekani weusi hawawapendi Waafrika?Na pia ni kwanini wanajiona bora kuliko waafrika?Nisaidie maana najua wewe upo jikoni kabisa.Pitia makala yangu ya Lessons from Hurricane Katrina,So far.Ipo kwenye blog yangu.

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com