11/12/2005

TATIZO NI WA-TWAWALA AU WATAWALIWA?

Tatizo kubwa kabisa Tanzania na pengine bara zima la Afrika watu wengi hudhani kuwa ni wa-twawala. Hapana. Tatizo namba moja ni watawaliwa. Wao ndio tatizo kubwa kuliko wanaowatawala. Watawaliwa ni wengi lakini wanakubali kunyonywa na kudanganywa na kundi dogo la watu fulani (wengi wakiwa ni wanaume).
Lakini kundi hili dogo nalo linajua kuwa udogo wake unaweza kuwatia hatarini kwahiyo linaunda vyombo kama polisi, magereza, sheria, mahakama, n.k. Vyombo vyote hivi kazi yake ni kuwalinda. Unadhani kazi ya FFU ni nini? Kazi yake ni kuzuia wananchi kuamka na kuleta mabadiliko. Wananchi wakitaka kutoa madai hadharani au kwenda kuwafuata huko wanakokaa, FFU kazi yao ni kuzuia.
Kila siku polisi wanakamata watawaliwa kwa madai ya uvunjaji sheria lakini huoni hata siku moja polisi hao wakikamata au kupiga mabomu ya machozi watawala. Ina maana kuwa watawala Tanzania au Afrika hawaibi? Hawaui? Hawavunji sheria? Au sheria huwa zinavunjwa na watawaliwa tu? Watawala wakivunja sheria ni sawa. Watawala wetu wanaiba. Wanaua. Wanatesa. Wanatumia vyombo nilivyokutajia.
Kama wahalifu halisi walikuwa ndio wanakamatwa, watawala wengi walioko madarakani wangetakiwa kuwa jela kwa miaka mingi sana.
Kundi hili dogo linapotumia vyombo vta dola kuwaweka ninyi mlio wengi chini ya himaya yake, wanatumia mfumo wa elimu na vyombo vya habari kukuhadaa uamini kuwa bila wao jamii haitakalika. Wanakufanya udhani kuwa maendeleo yako wao ndio watayaleta. Unakutana nao wakati wa kampeni wanasema kuwa watawaleteeni shule, maji, elimu, n.k. Ahadi zinazotolewa na wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi zingekuwa zinatekelezwa, Tanzania ingekuwa nchi ya kuigwa na dunia nzima.
Kukiwa na jamii ambayo inadhani kuwa maendeleo atayaleta mtu mmoja ambaye kazi yake mwaka mzima sio kuzalisha kitu bali kujaribu kukushawishi umpe kura, jamii hiyo inapaswa kuzinduka mapema.
Wa-twawala wakishatupata hapo kwenye imani kuwa bila mfumo wa utawala ambao unawapa wao (wachache) nguvu kubwa zaidi yetu (tulio wengi) nchi haitapata maendeleo, wanatukamata kwenye imani nyingine potofu. Imani hiyo ni kuwa bila polisi, magereza, mahakama, sheria, wanajeshi, n.k. jamii haitakalika. Watu watauana na kuibiana.
Kama ni kweli kuwa polisi, mahakama, magereza n.k. kazi yake ni kujenga jamii isiyo na uhalifu, basi nchi zenye polisi wengi na wenye dhana za kisasa kama Marekani, mfumo wa mahakama uliokomaa, magereza yenye ulinzi mkali zingekuwa hazina uhalifu. Pengine unaweza kudhani nimepungukiwa nikisema kuwa kazi ya polisi sio kuondoa uhalifu na kuhakikisha jamii inaishi kwa amani. Nadhani unapaswa uokoke kwanza ndipo ukubaliana nami. Kuokoka kwenyewe sio kama kwa Askofu Kakobe. Kuokoka kwa tofauti.
Usiniambie kuwa na mahakama unadhani kazi yake ni kutoa haki. Kazi yake ni kulinda haki ya mwenye nacho dhidi ya asiyenacho. Haki ya wa-twawala dhidi ya watawaliwa. Niambie, kuna wa-twawala magerezani? Kuna wenye nacho magerezani? Magerezani wengi ni wale wenzetu wenye kuvaa malapa. Je ina maana kuwa wavunja sheria ni watawaliwa tu? Kama unafikiria kama mimi utakubaliana nami kuwa walioko mahakamani, polisi, wanaopitisha hizo sheria pengine ndio walitakiwa kujaza magereza kama haki ingekuwa inatendeka.
Kundi hili dogo la wa-twawala limefanikiwa kwenye jambo moja kubwa sana. Wameweza kutufanya tuamini kuwa hata kama hatuwataki hakuna njia ya kuwaondoa kwenye usukani. Wanatumia sheria kadhaa kutisha watu kuandika maoni yao kama haya ninayoandika hapa. Sheria hizo zinawapa nguvu za kutia watu ndani wanaoelimisha umma juu ya mfumo wa kibabiloni unaonyoya damu ya watawaliwa. Wanaweka sheria ambazo inakuwa vigumu wewe kuungana na wenzako ii kuwaondoa kwenye usukani.
Napenda kukuhakikishia kuwa mfumo huu wa kibabiloni, mfumo wa kihaini unaoneemesha tabaka la wa-twawala huku maelfu ya wananchi wakiwateseka kwa tabu na umasikini uliokithiri, unaweza kuondolewa kwa sayansi ndogo sana. Sio tu unaweza kung'olewa, bali unapaswa kung'olewa.
Usiutii.
Usiutii.
Usiutii.

3 Maoni Yako:

At 11/13/2005 01:10:00 AM, Blogger Indya Nkya said...

Pa kuanzia ni kuwaelewesha kwamba hao polisi, jeshi na wengineo kwamba nao ni watawaliwa. Si watawala. Wangekuwa watawala wasingelala nyumba za bati au kulala getini kwa waziri akiwa ameshikilia bunduki usiku mzima. Inabidi pia wote tukubali tuvunje tabaka moja. Wote tuwe watawala au watawaliwa. Tukishawaondoa hao jamaa hapo katikati wanaowalinda watawala basi tutakuwa karibu kuondoa matabaka. Unajua kwa mfano maandamano kama yale ya Ukraine yaliyoondoa jamaa ni kwamba walinda watawala si kwamba walizidiwa nguvu. Ilifika mahali nao wakajiona wapuuzi kwamba na sisi hatuna tofauti na hao wanaoandamana. Japo nao waliandamana kumwaka mtwawala mwingine. Kuna upuuzi mkubwa sana wa watwawala kujisifu na kuahidi kujenga barabara na mengineyo. Hivi wanatoa pesa mfukoni? Wanabeba zege au watajengaje barabara. Nachanganyikiwa kiasi

 
At 11/13/2005 01:26:00 AM, Blogger Innocent Kasyate said...

Kama ilivyo vigumu kumfanya mtu kuamini kuwa hakuna Mungu basi ndivyo hivyo kwa wananchi wengi tena maskini wasichoka kuendelea kuamini kuwa bila watwawala hakuna maisha.
Watwawala wanajua wananchi wengi walivyo wajinga ndio maana wako kama wanavyofanya.
Ndesanja unasema tuandamane tuwatoe kwa nguvu aise, polisi watatuua.Nakwambia majeshi yetu polisi na wale wa ulinzi kumejaa watu wasiokuwa na akili timamu. Unajua jeshi la polisi kule kwetu linaongozwa na kijeba cha darasa la saba?
Fikiria mwenyewe
Tumekwisha.

 
At 11/13/2005 03:21:00 PM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Nkya,
Hata mimi nachanganyikiwa kabisa. Zege watabeba?

Inno, nadhani ili hao wakuda wasitupige risasi itabidi tufanye Nkya anachosema: tuwaelimishe kuwa haki tunazodai ni haki zao pia na ndugu zao, watoto wa watoto wao, wazazi wao, babu na bibi zao, n.k. Tunadai haki zao ili walipwe ujira halali. Wapewe nyumba bora za kuishi na sio nyumba za mabati na "kota" zilizosongamana, vyumba vidogo, familia kubwa...msongamano ndani ya nyumba unaweza kufikiri uko soko la Kariakoo au soko la Kiboriloni siku "mabela" ya mitumba yakifunguliwa.

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com