12/13/2005

Mkutano wa wanablogu, changamoto, tufanye nini?

Mkutano wenyewe ulifanyika tarehe 10 Desemba. Wanablogu toka pande mbalimbali za dunia walikutana katika makao makuu ya shirika la habari la Reuters (wakiwemo Paul Kihwelo wa kitivo cha sheria Chuo Kikuu Huria Tanzania, ambaye blogu yake itakuwa hewani karibuni na Fatma Karama). Mambo kadhaa yalijitokeza ambayo yanatuhusu wanablogu wa Kiswahili. Mawili makuu: 1. Jinsi gani ya kuongeza idadi ya blogu? 2. Je mradi wa Sauti za Dunia ufanye nini kuhusu blogu ambazo sio za kiingereza?
Ningependa tutazame hayo masuala mawili na kujadiliana kitu/mambo gani tunaweza kufanya. Tayari nimejadiliana kwa kifupi na Jeff na Paul. Mawazo yetu wote yanahitajika. Jambo mojawapo ambalo Jeff nami tumeligusia ni kuwa tunaweza kupeana changamoto: kila mwanablogu alete wanablogu wawili wapya...wawili tu...kwenye blogu za Kiswahili. Paul Kihwelo amezungumzia umuhimu wa sisi kukutana. Alizungumzia jambo hili kwa kirefu alipokutana na Ethan Zuckerman, mmoja wa waanzilishi wa Sauti za Dunia. Na anaporudi Tanzania atalifanyia kazi.
Wakati huo huo kuna "wiki" ambayo imeundwa kwa ajili ya kubunga bongo na kukusanya mawazo kuhusu nini cha kufanya ili kuimarisha mradi wa Sauti za Dunia na kupanua wigo wa blogu duniani. Unaweza kuchangia mawazo yako. Kuhusu suala la lugha na tafsiri bonyeza hapa. Kuhusu suala la kuongeza na kuvutia watu zaidi katika ulimwengu wa blogu, bonyeza hapa. Ukitaka kuona "wiki" nzima bonyeza hapa.
**Wiki: wiki ni aina ya teknolojia ambayo inaruhusu ukurasa wa kwenye tovuti kuhaririwa au kuandikwa na mtu yeyote bila haja ya kuwa na neno la siri au ufahamu wa lugha ya kompyuta kama "html." Teknolojia hii ndio tunayotumia katika kutengeneza kamusi elezo ya Kiswahili. Ukibonyeza hapa utaiona kamusi hiyo na unaweza kushiriki kuiandika. Pia kwa wale ambao nimewahi kuwagusia kuhusu mradi ule ninaosimamia wa kuandika katiba kwa kutumia "wiki," basi teknolojia yenyewe ni kama hii.
Rebecca MacKinnon, mmoja wa waanzilishi wa mradi wa Sauti za Dunia, ameandika muhtasari mzuri sana wa mkutano huo wa wanablogu. Tafadhali ukiwa na muda usome ili tusije kupitwa na mazungumzo yanayoendelea duniani kuhusu blogu. Bofya hapa usome muhtasari huo.

2 Maoni Yako:

At 12/16/2005 07:37:00 PM, Blogger Jeff Msangi said...

Ndesanjo,
Bado nasubiri wanablogu wenzetu waweke mawazo yao hapa juu ya nini kifanyike.Labda ungerudia tena huu ujumbe kwa sababu naamini hili ni suala muhimu sana hususani wakati huu ambapo upinzani huko Tanzania umeshindwa kabisa kufurukuta.Blogu ni vuguvugu letu la kijamii.Tunachotakiwa kufanya hivi sasa ni kuhakikisha uwajibikaji kwa hawa viongozi.Lazima wawe watumishi wa umma na sio vibosile wa wananchi.

 
At 12/17/2005 07:41:00 AM, Blogger Mija Shija Sayi said...

Baba Ukweli,
Nakubaliana na wazo la kila mwanablogu kutafuta wanablogu wawili wapya ili kuongeza idadi yetu. Lakini pamoja na wazo hilo unaonaje kama tungetumia na mbinu nyingine ya "kuwasiliana moja kwa moja na vyuo na mashule ya Tanzania kwa kutafuta tovuti zao na kuwaandikia juu ya suala zima la Blogu na umuhimu wake. Halafu utawala wa shule ndio uwahimize wanafunzi wake, na kwa vile siku hizi karibu mashule yote yana kompyuta wataweza kuona mfano halisi wa blogu zenyewe na jinsi zinavyofanya kazi. Nina hakika kuna wafurukutwa wengi sana mashuleni ambao hadi sasa hivi hawajui ni wapi pa kutolea sauti zao (hasa hasa wanafunzi walioko vijijini). Sasa wakipata nafasi hii hawataichezea.

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com