12/13/2005

Waulizeni Kituo cha Haki za Binadamu, hao "binadamu" ni akina nani?

Majuzi niliandika kuhusu Tuzo ya Haki za Binadamu ya Majimaji aliyopewa Jaji James Mwalusanya. Kama hukusoma niliyoandika, bonyeza hapa usome. Tuzo hiyo ilitolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu. Niliwapongeza kwa kumpa Jaji Mwalusanya tuzo hiyo kutokana na mchango wake katika ujenzi wa demokrasia Tanzania kupitia maandiko yake na hukumu mbalimbali ambazo amewahi kutoa.
Lakini nikawanyooshea kidole wanaharakati hawa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kosa ambalo linatokana na ugonjwa ambao inaelekea ni mbaya kuliko ambavyo wengi tunadhani. Ugonjwa huu ni ule unaotufanya kutumia lugha ya kiingereza hata pale ambapo walengwa wetu lugha yao kuu ni Kiswahili. Tazama majina ya mashirika yasio ya kiserikali, vyama vya upinzani, kampuni za kibiashara, maduka, baa, bendi, na hata vikundi vya utamaduni. Utakuta majina ya kiingereza ndio yanaonekana kuwa ni bora zaidi.
Achilia mbali majina, tuje kwenye tovuti. Nimeongelea kwa muda mrefu kuhusu tovuti ya ikulu, waziri mkuu, bunge, tume ya uchaguzi, mwanablogu mmoja (sijui alikuwa ni Nkya au Egidio) akatukumbusha pia tovuti ya Makumbusho ya Taifa, n.k zina taarifa muhimu kwa Watanzania kwa lugha ya kiingereza. Niliwahi kusema kuwa iwapo Rais akiongea na Watanzania anatumia kiingereza basi sitalalamika iwapo tovuti ya ikulu ni ya kiingereza. Iwapo wabunge ni wawakilishi wa wananchi ambao lugha wanayotumia asubuhi, mchana, na jioni ni Kiswahili, kwanini tovuti ya bunge lao na miswada ya sheria iwe ni ya kiingereza? Kama huu sio ugonjwa ni nini?
Sasa nilipokuwa naongelea kuhusu Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, nikauliza: kuna sababu gani ya tovuti ya kituo hiki kuwa ya kiingereza wakati ambapo wanatuambia kuwa lengo lao kuu ni kuwawezesha Watanzania wasiojiweza kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, na kiroho kwa kuwapa mafunzo ya haki za binadamu na kuwapatia msaada wa kisheria? Kama nia ya kituo hiki ni kuwasaidia hao Watanzania, kwanini watumie lugha ya watu wengine na sio lugha wanayotumia Watanzania masaa 24?
Soma mwenye lengo kuu la kituo hiki (kwa kiingereza). Nimetoa kwenye tovuti yao (wino mzito nimeuweka mwenyewe):
The primary task of the Legal and Human Rights Centre is to create legal and human rights empowerment amongst the socially, economically, culturally and spiritually disadvantaged and marginalized groups within the Tanzania society through legal and human rights training, provision of legal aid, information generation and dissemination through publications and radio programmes, research on legal and human rights issues and networking and alliance building with other institutions which share this mission.
Nilipoandika kuhusu hili, mwanablogu Jeff, akatoa maoni yake akitaka kujua kama "binadamu" wanaozungumziwa na kituo hiki ni pamoja na babu na bibi yake kule Kilimanjaro. Alisema, "Huenda wanadamu wanaoongelewa hapa sio babu yangu na bibi yangu kule Kilimanjaro."Wanadamu" hawa nadhani ni wale ambao tayari wanazijua baadhi ya haki zao za msingi.Kituo kinafanya kuwakumbusha tu pale wanapoonekana kuzisahau."
Mwanablogu Da Mija akatoa wazo: "Mimi naona tuanze kuwaandikia moja kwa moja kuwauliza kwanini wanatumia kiingereza kuwaandikia waswahili, je wanajua madhara yake?"
Suala hili la lugha wengine wanaweza kuona kuwa ni jambo dogo sana. Hapana. Kama ambavyo tovuti ya shirika lisilo la kiserikali Uingereza haitakuwa ya Kiswahili maana hawatumii lugha hii ndivyo hivyo tunaamini kuwa tovuti ambayo inatoa taarifa, elimu, na maarifa kwa Watanzania haina haja ya kuwa ya kiingereza. Hili ni suala la kujikwamua. Kama tovuti hizi zinatengenezwa kwa ajili ya wafadhili, tuambiwe. Ila kama zinatengezwa kwa ajili ya kutoa taarifa na elimu kwa Watanzania, basi hakuna sababu ya kukopa lugha ambayo wengi tunaielewa kijuujuu. Ukitaka kujua lugha gani uitumie unapotaka kutawanya habari, taarifa, elimu, n.k. kwa Watanzania, nenda kwenye vituo vya mabasi, uwanja wa mpira, baa, saluni, vijiwe vya kahawa, mashambani, kampeni za kisiasa, n.k., tazama Watanzania wanatumia lugha gani sehemu hizo.
Kama Da Mija alivyosema, tunapaswa kuwaambia Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kuwa ni busara na heshima kwa taifa na utamaduni kujenga tovuti yao kwa Kiswahili. Haki za binadamu wanazotetea zinajumuisha pia haki za kitamaduni. Haki za kuwa na utamaduni wako, kuujua, na kuuheshimu.
Bonyeza hapa uone tovuti yao. Anuani yao ya barua pepe ni hii: lhrc@humanrights.or.tz
Na simu yao ni hii: 2773038, 277 3048

Bonyeza hapa usome moja ya makala zilizowahi kuandika kuhusu suala la kimombo kwenye tovuti za umma.

4 Maoni Yako:

At 12/14/2005 03:26:00 AM, Anonymous Anonymous said...

Umeshauri kuwa "tunapaswa kuwaambia Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kuwa ni busara na heshima kwa taifa na utamaduni kujenga tovuti yao kwa Kiswahili". Tujadiliane matumizi ya lugha yetu leo hii! miaka 44 baada ya kupata kile tunachokiita uhuru -- hili si suala la mjadala. Tukubaliane, wanaouwa nchi tena kwa makusudi mazima ni hao hao wanaoitwa wasomi, sababu ni nini lakini? utumwa?, pesa?, ulimbukeni? au vyote pamoja?

 
At 12/14/2005 06:25:00 AM, Anonymous Anonymous said...

kwa kweli mimi nimeona kujadili tu huku haifai nimeamua kutuma Email na kama hawakunijibu basi nitawapigia simu baada tu yakumaliza harakati za uchaguzi na ninaomba wana blog,wana kasri,wana jamaat wote kwa umoja wetu kutumia mwanya huu kuwaandikia barua pepe na kupiga simu huku tukiwaandikia ujumbe makala katika magazeti ya hapa nchini.ni wazi pia kujadili huku bila kufikisha ujumbe huu kwa jamii nzima(kwa wale wanaotembela internet na wale wanaosoma magazeti, ama kusikiliza kusikiliza redio na kuona katika runinga)itakuwa ni kazi isiyo na manufaa ya msingi na kuleta athari za wazi

 
At 12/14/2005 10:44:00 AM, Blogger Indya Nkya said...

Macha hizo jitihada lazima zizae matunda siku moja. Lakini nitazidi kukumbusha kila siku. Kama ulivyogusia nina imani kwamba tovuti nyingi ni za wafadhili si za akina mama kuluthumu na kina Majuto, Maganga, Masawe na wengineo.

 
At 12/23/2005 12:40:00 AM, Blogger FOSEWERD Initiatives said...

Bwana Ndesanjo,

naungana na ukweli uliomo kwenye makala hii pamoja na maoni ya wachangiaji wenzangu! je mbona hata microsoft wamekubali kuwa kiswahili ni muhimu na wamekiingiza kwenye mtandao? itakuwa hiyo tume? cha pili ni kwamba hapa ninaona juhudi za makusudi za watwawala kuweka elimu ya uraia mbali na wananchi ili washishe net na kukoroma! hili lazima tulipigie kelele! haiwezekani eti mgombea ubinge aseme polisi ni mali a chama twawala miaka 44 baada ya uhuru MHALIFU MKUBWA! sina uwezo tu kwa sasa ila ninadhani umefika muda wanablogu tuanze kampeni ya kuwafikisha mahakamani wale ambao wanaongeza ujinga badala ya kuongeza uelewa wa wananchi kwa haki zao. pia wanablogu, tutafakari haya mambo mengine, je ni nani anawasemelea wale waliozuia mamluki wakaishia kupigwa kule unguja? je hatuwezi kuchukua hatua zozote kisheria? maana naona hao waliojiwekea mtandao kwa kingereza hawana mpango wowote na hilo! HAYA MAMBO NI LAZIMA TUNYOOSHE KWA FAIDA YETU NA VIZAZI VIJAVYO! si kwa ajili ya Amani wala Kikwete!

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com