1/09/2006

Nikisomwa na Mwalimu Mmoja Kama Bwaya Inatosha

Bwaya kaniuliza swali swali zuri sana. Anataka kujua kama makala zangu (ambazo baadhi ziko ndani ya blogu hii, upande wa kuume chini ya picha yangu) na za wengine zinasomwa na Watanzania? Bonyeza hapa usome aliyoandika. Bofya hapa usome swali lake jingine kuhusu makala zangu.
Sijui nijibu swali lake la makala zinasomwa au la kwa upande gani. Ngoja niseme hivi: historia ya mabadiliko ya jamii duniani inaonyesha kuwa kundi dogo sana huwa ndio linaongoza mabadiliko hayo. Kwahiyo unapotaka kuleta mabadiliko unaweza kuwa umegusa watu wachache sana. Muhimu ni aina ya watu uliowafikia. Kwa mfano, walimu kama wewe. Kitendo cha kuwa wewe utakuja kuwa na kazi ya kutengeneza fikra na akili za vizazi vijavyo kimenifanya nifurahi sana kujua kuwa unasoma makala zangu. Hata kama nchi nzima ni wewe peke yake unazisoma, nitaridhika kabisa maana najua kuwa idadi ya watakaosoma makala zangu kupitia wewe (yaani kutokana na mafunzo na maarifa utakayowapa uliyoyapata kwenye makala zangu) ni wengi. Ninatazama jambo hili kwa misingi hiyo.

Lakini pia makala inaweza kusomwa na watu watatu, ila kwakuwa tunaishi kwenye jamii ambayo bado ina utamaduni wa gumzo mtaani, kwenye mabasi, majumbani,n.k., wako wengi ambao hawajaisoma hiyo makala lakini watapata yaliyoko kwenye makala hiyo kupitia wale watatu waliosoma.

Nakubaliana na Bwaya kuwa watu wetu hawapendi sana kusoma masuala nyeti. Wanataka habari nyepesi nyepesi. Lakini napenda tuwatambue wale wachache wenye moyo wa dhati wa kujisomea masuala mazito. Wapo na wanaongezeka. Wapo na wanawavuta wengine. Wapo na kila siku nasoma barua zao pepe wanazoniandikia wakishukuru, wakitaka ufafanuzi zaidi, wakitoa mapendekezo ya mada wanazotaka niandike, wakinikumbusha mada nilizowahi kusema kuwa nitaziandikia na kadhalika.

Kuna wanafunzi ambao wanasoma makala zangu na kujadili katika vilabu walivyoanzisha viitwavyo Jikomboe. Kuna walimu wanaotumia makala hizo kufundishia. Kuna wazazi wananiambia kuwa wanazijadili na familia zao. Wako vijana wameanzisha vikundi mtaani vya kusoma makala zangu kwa pamoja na kuzichanachana (kuzichambua). Wako ambao pia wameitikia wito ambao nimekuwa nautoa mara kwa mara kwa vijana kuunda makundi ya kujadili masuala nyeti ya katiba, utamaduni, historia, n.k. Kundi moja la vijana hawa limeniandikia hivi karibuni kunikumbusha jambo nililozungumzia katika makala moja niliyoandika miaka mitatu iliyopita!

Kwahiyo makala zangu (na zile za akina Boniphace na Jeff) wanaweza wasisome Watanzania wote, ila kumbuka kuwa wale wanaosoma wanaishi miongoni mwa Watanzania ambao kwa namna moja au nyingine wanakuwa kama wamezisoma kupitia mijadala, mabishano, gumzo, n.k., na wale waliozisoma.

Lakini narudia kusema kuwa watu wachache ndio huleta mabadiliko. Au niseme, watu wachache huongoza mabadiliko. Halafu niseme kuwa kama ninasomwa na mwalimu mtarajiwa Bwalya...ninajisikia kuwa kazi yangu sio bure. Hata wasiponisoma Watanzania wote. Mwalimu mtarajiwa mmoja anatosha kabisa.

Kuhusu utamaduni wa kujisomea, kweli hili ni tatizo kubwa nchini kwetu. Utatuzi wake unahitaji juhudi zetu binafsi kwenye familia, juhudi za watunga sera, taasisi, na serikali. Ukitaka kujenga utamaduni wa kujisomea wa nchi nzima utakata tamaa. Usianze na nchi. Anza na waliokuzunguka. Kama hujaweza kujenga utamaduni wa kujisomea wa watoto jirani zako au ndugu zako, huwezi kuanza kufikiria nchi. Utamaduni wa kujisomea wa nchi unaanza kujengwa majumbani, mitaani, nyumba kumikumi, n.k., kasha unakuja kuwa utamaduni wa taifa. Nakumbuka mimi kaka yangu alinisaidia sana kuwa na ari ya kujisomea. Nikiwa darasa la pili alinipeleka maktaba ya mkoa mjini Moshi akaniandikisha nikawa mwanachama. Toka wakati huo hadi leo nimekuwa “mgonjwa” wa kujisomea. Siku hizi nasoma kitabu zaidi ya kimoja kwa wakati mmoja (sina maana dakika hiyo hiyo).

Basi kitendo cha kaka yangu kunifanya nitambue utamu ulioko ndani ya kurasa za vitabu. Nikatumbukia kwenye kujisomea vitabu hadi ikafika wakati nikawa najifanya kuwa naenda shule kumbe nakwenda maktaba, shule siendi. Maktaba nilikuta vitabu ambavyo vilinigusa sana tofauti na vitabu vya shuleni. Masomo shuleni na vitabu tulivyokuwa tukitumia vilikuwa kama pombe ya mbege iliyotiwa maji. Masomo shuleni yalikuwa hayanipi changamoto. Sisemi kuwa huu ni mfano wa kuigwa ila nataka kuonyesha tu jinsi ambavyo nilijawa na hamasa ya kujisomea baada ya kaka yangu kunifungua macho. Toka wakati huo, ukitaka kunipata nenda maktaba au maduka ya vitabu. Utanikuta kwenye kona nimejikalia sakafuni ninachimba. Mji wowote ninaokwenda. Nchi yoyote ninayokwenda.

Kwahiyo tuna wajibu wa kuanza kubadili wale watu waliotuzunguka. Watoto wa jirani yako, watoto wa kaka yako, ndugu wa kuzaliwa tumbo moja, washikaji zako mtaani, n.k. Nikifanya hivyo, na yule akafanya hivyo, na wale nao, ndivyo tunabadili nchi.

Lakini pia tusidharau kabisa nguvu ya vyombo vya uongo (habari). Kuna nguvu nne duniani ambazo ndizo zinatufanya tuwe kama tulivyo. Nguvu hizi ndio zinatujengea mtazamo tulio nao kuhusu maisha: vyombo vya uongo/habari, dini, utamaduni-maarufu, na mfumo wa elimu.

Nje ya hapo hakuna kitu. Sasa tunaweza pia kutumia nguvu hizo hizo kupindua hali ilivyo na kujenga jamii mpya. Tunaweza kujenga hiyo jamii mpya hata tukifikia asilimia 0.5 ya Watanzania wote. Hasa walimu kama Bwalya. Fikiria mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi wangapi katika uhai wake. Sasa ukifikia mwalimu mmoja ni sawa na kufikia idadi ya wanafunzi atakaowafundisha. Na hao wanafunzi atakaowafundisha kuna ambao watakuwa walimu. Nao watafundisha wanafunzi wangapi? Na kuendelea.

4 Maoni Yako:

At 1/09/2006 05:04:00 AM, Blogger FOSEWERD Initiatives said...

kaka ndesanjo,

naomba niongeze hapo. kuna watu wengi sana ambao wanafuatilia mada hizi lakini bado hawajajishughulisha kufungua blogu zao, kama unavyojua watz wengi hawapendi sana risk, au ni late adopters. mfano hapa nilipo watz wote walio katika hii institute wanafuatilia hizi blogu na kusoma makala kila siku japo hawachangii kwa kuandika ila kwenye vikao vya bia huchangia na wamezisifu sana! suala hapa ni kuwa impact ipo tena ni kubwa sana!

uhuru!

 
At 1/09/2006 10:07:00 AM, Blogger boniphace said...

Mwaka umeanza Ndesanjo anayedhani hakuna mwamko wa kusoma mwambie anadanganywa. Kama wananchi wangekuwa hawasomi ingekuwaje Magazeti yampambe Kikwete na wao waitikie ndio mzee. Tatizo ni moja hawajapata chombo mbadala lakini si kuwa hawapendi kusoma. Kuna haja pia ya kuisoma hadhira yako kabla hujaiandikia! Hapa tutaanza baada ya kuwa wengi lakini sasa bado tuko katika wakati wa kufunua fikra na kubatiza umma. Hakuna kukata tamaa, cheza karata yako.

 
At 1/10/2006 07:39:00 AM, Blogger Christian Bwaya said...

Mloyi kaniandikia, anasema Ndesanjo anatumia nguvu nyingi kuandika makala hizo ( lengo likiwa ni la kizalendo kabisa, kuwabadilisha wanajamii). Wasiwasi wake ni kama wasomaji wanajishughulika kuuelewa vizuri ujumbe anaokuwa anataka uifikie hadhira. Hii ni changamoto hata hivyo.

 
At 1/10/2006 08:32:00 AM, Blogger Christian Bwaya said...

Nilifurahi kusoma makala yako kwenye Mwananchi Jumapili. Nilipenda sana ulivyojibu hoja kwamba sikukuu zote zimetungwa na watu.
Mimi ni Mkristo. Lakini kuwa Mkristo hakunifanyi nisihoji baadhi ya mapokeo ya kanisa ambayo kila ninaposoma biblia sikuti mahala yanaonekana.
Ulimalizia makala yako kwa kuwauliza wasomaji wako kama wanaweza kumsaidia. Nikiri kwamba haiwezakani kumsaidia. Kuanzia mwanzo wa kitabu cha Biblia mpaka mwisho hakuna mahala panapoelekeza hivyo.
Ukisoma historia ya Krismas utaona kuwa ni siku ya kutunga, na walioitunga wameiweka katika namna ambayo wengi hawawezi kujua kuwa wamedanganywa. Afadhali ulisema ni ya wazungu, maana ndivyo ilivyo!
Sisemi tusisherehekee. La, tusherehekee lakini tukijua kuwa ni utunzi tu. Huo ndio ukweli.
Sikukuu ya Kwanzaa sikuwa naielewa. Lakini imenivutia. Watu wankumbushana historia yao. nadhani ni jambo jema ambalo naamini limefika Afrika sasa. Ila ile sehemu ya katambiko, sijaielewa vizuri.
Nikupongeze kwa makala zako nzuri. Ila nasikitika huwa siazimwi hata gazeti chuoni kwangu. Sijakata tamaa, lakini badiliko linahitaji muda zaidi ilki waanze hata kusikiliza mijadala ya jinsi yako.

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com