1/08/2006

Uzuri wa Ugonjwa Huu ni Kuwa Una Dawa. Tutautibu!

Nimesoma aliyoandika Chemi akitushauri kupenda urembo wa asili. Amezungumzia pia yale mashindano ya "miss world." Sijui nitasema nini katika waraka huu ila najisikia kuandika kidogo kuhusu hili suala na mengine yanayohusiana nalo. Bonyeza hapa usome Chemi aliyoandika Chemi. Chemi amehoji vigezo vinavyotumika kuchagua mwanamke mmoja kuwa ni mrembo kuliko wote duniani.

Kitendo tu cha dunia yetu ya leo kutumia muda na fedha ili watu washindane kuwa nani mzuri zaidi kinahitaji kuchambuliwa kwa kina zaidi. Ukiingia ndani sana katika uchambuzi wa suala hili utakuta masuala ya mwili wa mwanamke kufanywa kama chombo cha biashara, burudani (kwa macho na tamaa za mwili za wanamume), na mwili huo kuwa ni matangazo ya biashara. Kuna itikadi inayofanya yote hayo. Katika itikadi hii mwanamke anakuwa ni chombo kinachojumuisha tu mwili (matiti, miguu, macho, nywele, rangi ya ngozi, kucha, tabasamu, mwendo, n.k.). Akili na nafsi havina nafasi. Mfumo wa ubepari ulivyo na uchu wa kufanya kila kitu kuwa bidhaa umehamisha ukandamizaji wa wanawake kwa kuupa sura ya kibiashara ambayo inaficha makucha ya ukandamizaji au kuyapa sura mpya inayofanana na ukombozi. Utaona kuwa mwanamke wa nchi za magharibi anadhani kuwa haki zake keshazipata na kuwa mwanamke anayekandamizwa ni yule aliyeko nchi za Kiislamu au Afrika wakati ambapo mwili wake (mwanamke huyo wa magharibi au yule wa Afrika anayetaka kujifanyakama huyo wa magharibi) umekuwa ni malighafi ya mfumo wa kibepari ambao bado unaongozwa na itikadi ya mfumo dume. Kama jinsi ambavyo mashirika ya umma yanavyobinafsishwa ndivyo mwili wa mwanamke unabinafishwa katika mfumo wa soko. Kinachobakia ni kuwa mwanamke anaonekana katika jamii kutokana na mwili wake na mwanaume anaonekana kutokana na anayofanya na fikra zake. Mtazamo huu unaotokana na kasumba ya mfumo dume ndio unafanya magazeti mengi kutoa safu maalum kwa waandishi au wanasafu wanaume. Na wanawake wachache wanaopewa safu wanatakiwa kuandika tu masuala ya haki za wanawake (ambapo kwa upande mmoja sio jambo baya lakini kunakuwa na mtazamo kuwa wanawake hawawezi kuongelea masuala mengine mazito kwenye jamii zaidi ya haki za wanawake).

Sasa turudi kwenye dhana kuwa dunia inaweza kumpata mwanamke mrembo duniani. Swali linakuja: mwanamke huyo atapatikanaje wakati ambapo vigezo vya urembo vinatofautiana katika mataifa na tamaduni mbalimbali? Wakati unawaza kuhusu swali hilo utajikuta ukisema kuwa tatizo sio tu vile vigezo vya kimagharibi vinavyochukuliwa kama ndio vigezo vya "dunia." Utaanza kuhoji pia mantiki ya mwanamke kupita mbele ya wanaume na wanawake na nguo ya kuogelea (tena wakati akiwa haendi kuogelea!). Au kama nilivyosema hapo awali, mantiki nzima ya kushindana eti nani mzuri zaidi duniani. Tunarudi kwenye hoja ya mwanamke kuwa ni chombo. Kuwa bidhaa kama vile mche wa sabuni au gari. Chini ya msukumo wa soko na mfumo wa utamaduni-beberu unaoendesha mashindano kama "miss world" falsafa ya mtazamo kuwa mwanamke ni chombo cha burudani kwa mwanaume na pia ni kama bidhaa sokoni imejificha chini utamaduni-maarufu unaotufanya tuone kuwa mashindano hayo ni sehemu tu ya burudani inayofurahisha na kutufanya tufurahie maisha. Na wakati mwingine anayeshinda au kukaribia kushinda akiwa ni mtu wa kwetu, tunajenga imani nzito kabisa kuwa mashindano hayo ni tukio muhimu sana duniani. Utamaduni huu unafanya sehemu kubwa ya maisha kuwa ni kama vile tamthilia ndani ya luninga, maisha ni aina ya kujirusha katika bahari ya umagharibi. Utamaduni huu unafanya itikadi ya soko na utamaduni-beberu vinakuwa sio rahisi kuonekana.
Katika dunia hii ambayo maisha yanakuwa sawa na tamthilia ya kwenye luninga au kituko fulani, masuala ya maarifa, heshima ya utamaduni mseto, mijadala ya masuala ya msingi kwa wanadamu na jamii endelevu havina nafasi yoyote. Ndio maana inakuwa rahisi kwetu kufuatilia mashindano ya "miss" world kwa karibu zaidi kuliko Mkutano wa Jamii-Habari uliofanyika Tunisia mwaka jana. Ndio maana ni rahisi kwetu kufuatilia kwa furaha na hamasa iliyokaribia kuwa uendawazimu vituko vya kwenye luninga kama Big Brother au habari za udaku magazetini. Ndio maana ni rahisi zaidi kujua nani kashinda mashindano ya “miss” Tanzania zaidi ya jina la mwanafunzi aliyepata maksi za juu kabisa kwenye mtihani wa kidato cha nne. Ndio maana ni rahisi kufuatilia kwa shauku nani atashinda “miss” world kuliko nani atapata tuzo ya Nobeli ya Amani.

Kuna itikadi ndani ya haya yote. Itikadi hii ndio iliyofanya kifo cha Diana (aliyewahi kuwa mke wa mwana wa mfalme wa Uingereza, Charles) kuwa ni tukio kubwa kabisa kwa zaidi ya wiki moja huku kifo cha Mama Tereza (aliyefariki kipindi hicho hicho) kuwa ni habari za ukurasa wa ndani kwenye magazeti na habari za sekunde au dakika kadhaa kwenye luninga zilizokuwa zikirusha matangazo ya Diana asubuhi, mchana, jioni. Ni falsafa hii, tunaporudi kwenye suala la mwanamke, inafanya matangazo mengi ya biashara kuwa yana picha za wanawake maana miili yao ni kama kitega uchumi kwenye mfumo wa soko. Miili yao inaweza kuongeza idadi ya wateja wako, kama wanavyoamini watengeneza matangazo.

Turudi kwenye suala la Chemi la vigezo. Nani kasema kuwa dunia inaweza kufikia makubaliano juu ya uzuri wa mwanamke na hata wa mwanaume? Tafsiri na vigezo vya uzuri vinatokana na utamaduni, mazingira, na wakati. Tamaduni tofauti zina vigezo tofauti. Katika vigezo hivi hakuna kigezo bora zaidi ya kingine. Kwahiyo vigezo vya ulimbwende ni tofauti kati ya jamii na jamii ila sio kuwa kuna bora zaidi ya kingine maana kila kigezo kinakidhi mahitaji ya jamii yake. Vigezo vya jamii moja vinaweza visiwe na maana yoyote ukivihamisha kwenye jamii nyingine. Ila kigezo ni bora kwa yule aliyeko kwenye utamaduni uloizalisha kigezo kinachotumika. Inaweza ikatokea kutokana na sababu za utumwa kitamaduni na kifikra, jamii moja ikadhani kuwa vigezo vyake ni vya ovyo na kutaka kuiga vigezo vya wengine kama tunavyofanya sisi. Huu ni ugonjwa, tena mbaya sana lakini uzuri wake ni kuwa una dawa.

Kama mnavyojua, wazungu na waarabu kwenye jamii za mwambao wamekuwa wakitupeleka puta miaka na miaka. Puta hii wamemkuwa wakitumia mbinu na mifumo mbalimbali. Karibu ukitazama kila upande utaona putaputa hii ya wazungu na waarabu. Putaputa ya kutufanya tujisahau, tujione kuwa sisi si kitu, sisi ni washenzi, na wao ni bora na mfano wa kuigwa. Kwahiyo mila na desturi zao zinafaa kuigwa zote bila kujali kama zina faida au la. Dini zao ni za kweli na zetu ni za uongo. Manabii wao ni wa kweli na wa kwetu ni wa uongo.
Juzi nimeweka maoni kwenye picha ya baraza la mawaziri iliyoko kwenye blogu nzuri ya picha ya Michuzi. Katika picha hiyo mawaziri wetu walivyovaa ukikata vichwa vyao ukaulizwa useme mawaziri hao ni wa serikali ya nchi gani huwezi kujua. Hawaonyeshi kabisa kuguswa na hisia za utaifa na azma ya kutangaza na kuheshimu utamaduni wetu kupitia mavazi. Gadaffi, ambaye ni mwarabu, siku hizi anatangaza mavazi yetu zaidi ya sisi wenyewe. Maoni niliyotoa hapo ni haya:
Mavazi ya mawaziri wetu yanasema mengi kuhusu fikra zao, athari za elimu (maana sio unaona kuna madokta na maprofesa?), athari za msukumo wa utamaduni-maarufu wa magharibi na mustakabali wa utamaduni utaifa wetu. Hata waziri wa utamaduni naye pia?? Lakini sijui nashangaa nini wakati jina lake (Seif Khatib) linaonyesha amevaa begani mwake utamaduni wa akina nani
.
Utaona kuwa nilikuwa nashangaa kuwa hata waziri wa kulinda na kuendeleza utamaduni wetu hakuvaa vazi la utamaduni anaotakiwa kuulinda na kuuendeleza. Lakini katika kushangaa huko nikakuta najishangaa mwenyewe kwa kumshangaa waziri huyo kwani hata jina lake mwenyewe halijatoka katika utamaduni anaotakiwa kuulida na kuuendeleza. Kama jina lake tu ni la kuazima kwanini nitegemee avae mavazi ya kutukuza utamaduni usio na jina linalomfaa? Anaitwa Seif Khatib. Yaani waziri wetu wa utamaduni amebeba jina la kiarabu huku akiwa “anaendeleza na kulinda” utamaduni wetu. Ugonjwa huu, uzuri mmoja, unatibika. Tutautibu kwa njia yoyote ile. Bonyeza hapa uone picha hiyo kwa Michuzi.

Tutazame mifano zaidi ya gonjwa hili baya lenye dawa. Mifano: unaweza kwenda Rombo ndani ndani kabisa, ukakuta duka limepewa jina la kiingereza wakati ambapo mwenye duka na wateja wake hawafahamu kiingereza sawasawa. Tazama vikundi vya sanaa za maonyesho. Wakati vikundi hivi kazi yake, kama katiba zao zinavyosema, ni kuendeleza utamaduni wa Mtanzania na Mwafrika, majina yao ni ya kiingereza. Unakutana na Tanzania One Theatre, Muungano Cultural Troupe, OYA Theatre Group, Chemchem Art Group, Albino Revolution Cultural Troupe, Chang'ombe Youth Center, Nyunyusa Dancing Troupe, Roots and Kulture, n.k.

Kitendo cha kudai kuendeleza utamaduni wa Mtanzania au Mwafrika na kushindwa kabisa kupata jina la kundi toka katika utamaduni unaouendeleza ni kielelezo cha jinsi gani ugonjwa unaotokana na ukoloni mamboleo, ukoloni uchwara, na ubeberu wa kitamaduni ulivyotuathiri. Kwahiyo usishangae unapoona eti "miss" Afrika akiwa ni yule mrembo aliyechaguliwa na wazungu na kwa kutumia vigezo toka katika tamaduni zao na msukumo wa soko na itikadi za kibepari. Msukumo huu wa soko unatoka pande nyingi ikiwemo pamoja na makampuni ya nguo, vipodozi, kampuni za madawa, mahospitali (yanayofanya upasuaji wa kupunguza watu unene), makampuni ya matangazo, vyombo vya uongo (habari), n.k. Makampuni yote haya yanafaidika kwa namna moja au nyingine dunia inapokuza vizazi vyake kwa ndoto kuwa mwanamke mwembamba ndiye kilele cha uzuri. Kwa maneno mengine, mfumo wa kibeberu unafaidika sana na ugonjwa tulionao Waafrika. Na kama mnavyojua mfumo huu umekuwa ukitutumia na kutumia rasilimali zetu miaka na miaka huku ukijibadili kutokana na upepo wa wakati. Kulikuwa na wakati wa ukabaila, ubepari, na ubeberu. Mifumo hii ndio ilizalisha utumwa, ukoloni, ukoloni mamboeo, utandawizi (kuna tofauti kati ya utandawazi ambao ni mpana zaidi na utandawizi ambao ni mfumo unaoendeshwa na itikadi inayotaka dunia nzima kutawaliwa na kundi dogo la wanaume wa kizungu wanaoishi Ulaya na Marekani).

Niishie hapa. Siku kama leo ni zile siku ninapoandika bila kujua hasa ninaelekea wapi na nitaishia wapi. Kama nimezurura huku na kule bila kuishika mada sawasawa nisamehe. Huu ulikuwa ni mtiririko wa hisia na fikra. Kumbuka hii ni jumapili jioni na ninamsikiliza Bob Marley kwa sauti ya juu! Uhuru!

2 Maoni Yako:

At 1/09/2006 12:09:00 AM, Blogger mwandani said...

uzuri kitu cha moyoni. Mashindano ya uzuri ni soft porn iliyoidhinishwa kisheria, madhumuni yake ni yale yale.
Mie nafanya mashindano ya uzuri kila siku barabarani nikipiga shingo feni- Kumradhi akina dada, hasa kipindi hiki cha kiangazi huku matawi ya chini. Pesa wanazo lakini hawanunui nguo ndefu.
Uliyosema kweli, warembo wetu wangetaka kuwa wazungu hawatokuwa.

 
At 1/09/2006 05:17:00 AM, Anonymous Anonymous said...

Sisi ni wanyama wa kufugwa. Tumeshafugika na sasa hatujui kwetu ni wapi. Unakwenda mbali, tumechukuwa majina ya kigeni eti ni ya kidini, DINI ya nani? Toa miezi mitatu majina yote yabadilishwe. Tunazo Taifa STARS, Serengeti HEROES,ofisi za X- CONSULTANTS, Y-AND PARTNERS; Toa miezi mitatu zote zibadilishwe. Watu wanakoboa ngozi zao na kufunya nywele zao zifanane na za watu walio bora. Piga marufuku mikorogo na sana sana kwa mfanyakazi yeyote wa serikali iwe ni kigezo cha kujifukuzisha kazi. Tunasoma kwa lugha ya kigeni halafu tunaiita elimu; Masomo yaanze kufundishwa kwa kiswahili mara moja. Binti yetu ndo mzuri Afrika nzima! Mbona hawazidi hata wale wa mtaani kwake? Je, kwani anaweza kusonga ugali au kupika matoke chini ya dakika moja? Sasa huo uzuri ni upi. Je ushindi wake ni wa kweli au ni wa kutupa moyo tuendelee na mashindano tusiyafutilie mbali kama wakati ulopita? Anasifiwa kutangaza nchi na bendera yetu kabeba- kwa kutembea mbele za watu bila nguo?, Futa mashindano hayo mara moja.
Lakini tatizo ni pesa, huko kuna pesa kiasi kwamba vyombo vya habari na wasomi wetu (ajabu hata wale walosoma historia!) ndo waendelezaji wazuri wa huo utumwa.

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com